Vijana Sudan Kusini washambulia wafanyakazi wa kiutu, UN yalaani

30 Aprili 2021

Umoja wa Mataifa umelaani kitendo cha makundi ya vijana kushambulia wafanyakazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na yale yasiyo ya kiserikali kwenye mji wa Torit jimboni Equitoria Mashariki juzi Jumatano.

Msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya kibinadamu, OCHA, Jens Laerke amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo.

"Umoja wa Mataifa unalaani mashambulizi haya yaliyofanywa na vikundi vya vijana. Mashambulizi haya yametokea wakati kuna kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira nchini Sudan Kusini na matakwa ya vijana hao kuajiriwa na mashirika ya kibinadamu", amesema Bwana Laerke.

Baadhi ya mashirika, kwa mujibu wa msemaji huyo wa OCHA, yamelazimika kuhamisha wafanyakazi wao na kuwapeleka maeneo salama na hata maeneo ya kusafiri yamepunguzwa kutokana na ukosefu wa usalama.

"Operesheni za mashirika hayo zimesitishwa au zimepunguzwa ikiwemo huduma muhimu za afya na lishe. Uhamishaji wa wagonjwa mahututi kwenda hospitali ya taifa ya Torit, nao umevurugwa kutokana na kupunguzwa kwa shughuli za tiba mashinani huku baadhi ya vituo 40 ya lishe mjini Torit haviwezi kufikiwa na wananchi’" amesema Bwana Laerke.

Hali ya kibinadamu Equitoria Mashariki

Hivi sasa takribani watu 140,000 wana uhitaji mkubwa wa huduma za kibinadamu kwenye eneo hilo na mahitaji yao yanaweza kuongezeka zaidi iwapo wafanyakazi wa misaada, wengi wao raia wa Sudan Kusini, watashindwa kurejea kwenye majukumu yao kutokana na ukosefu wa usalama.

Mashirika yasiyo ya kiserikali, hivi sasa hayawezi kusambaza vyakula muhimu, huduma za afya, maji safi na huduma za kujisafi kwenye kaunti ya Torit. Bwana Laerke anasema bila hakikisho la usalama kutoka serikalini, makundi ya utoaji misaada kwenye mji huo yanaweza kushindwa kurejea tena kwenye operesheni zao.

Mratibu wa masuala ya kibinadamu nchini Sudan Kusini Alain Noudéhou anasema, "mashirika ya kibinadamu yanafanya operesheni zao Sudan Kusini kusambaza misaada muhimu kwa jamii zilizo hatarini zaidi. "Mashambulizi dhidi yao hayakubaliki na lazima yakome. Nasihi mamlaka na jamii ziwapatie hakikisoh la usalama na ulinzi wafanyakazi wa misaada na serikali isimamie sheria na utulivu."

 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter