Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mpango wa kurejea nyumbani kwa hiari waanza tena Libya baada ya kusitishwa kwa miezi 5

Wafanyikazi wa IOM Libya wakiwasaidia wanaosafiri  katika kituo cha meli  mjini Tripoli, Libya.
IOM
Wafanyikazi wa IOM Libya wakiwasaidia wanaosafiri katika kituo cha meli mjini Tripoli, Libya.

Mpango wa kurejea nyumbani kwa hiari waanza tena Libya baada ya kusitishwa kwa miezi 5

Wahamiaji na Wakimbizi

Wahamiaji 118 kutoka Ghana waliokuwa wamekwama nchini Libya na kushindwa kurejea nyumbani kutokana na janga la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19, wamerejea nyumbani kupitia mpango wa kurejea nyumbani kwa hiari. 

Hii ni mara ya kwanza kwa ndege hiyo ya kurejesha wahamiaji nyumbani kwa hiari kufanya safari yake tangu kusitishwa kwa mradi huo miezi 5 iliyopita kutokana na janga la Corona. 

Miongoni mwa waliokuwemo kwenye ndege hiyo iliyotua Accra, Ghana ni wanawake 7, watoto 3 na watoto wachanga 2. 

Taarifa ya shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM iliyotolewa mjini Tripoli nchini Libya imesema kuwa “IOM ilichunguza wasafiri wote walichunguzwa afya zao kabla ya kuondoka na walipatiwa vifaa vya kujikinga kama vile barakoa, glovu na dawa za kutakasa mikono sambamba na ushauri wa kisaikolojia.” 

Hata baada ya kufika Ghana, wahamiaji hao watawekwa karantini kwa siku 14, ambapo IOM itaendelea kuwahudumia n ahata kipindi cha kujumuika tena na jamii zao. 

Mradi wa kurejea nyumbani kwa hiari, VHR, umekumbwa na changamoto kubwa zaidi kutokana na COVID-19, mradi ambao umekuwa ndio kimbilio la wahamiaji wengi tangu uanze kutekelezwa mwaka 2015. 

Kutokana na COVID-19, kumekuwepo na vizuizi vikali kwa watu kutotembea nchini Libya ilhali IOM nayo inazidi kupokea maombi ya wahamiaji wanaotaka kurejea nyumbani kwa hiari. 

Zaidi ya wahamiaji 2,300 wamesajiliwa tangu mwezi Machi mwaka huu wakitaka kurejea nyumbani. 

Katika robo ya kwanza ya mwaka 2020, mradi wa VHR wa IOM umesaidia wakimbizi 1,466 waliokuwa wamekwama Libya, kurejea nyumbani. 

Mzozo nchini Libya sambamba na COVID-19 vimeathiri maisha ya wahamiaji ambapo tathmini iliyofanywa na IOM imeonesha kuwa asilimia 93 ya wahamiaji wameathiriwa na vikwazo vya kutembea na hivyo kukosa ajira na kutokuwa na uhakika wa kupata chakula.