Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yakidhi kiu ya wafugaji na wakulima huko Togo

Mradi wa FAO wa uhakika wa chakula (PESA) katika sekta ya kilimo, mifugo, maendeleo vijijini, uvuvi na kilimo
© FAO-Magnum Photos/Alex Webb
Mradi wa FAO wa uhakika wa chakula (PESA) katika sekta ya kilimo, mifugo, maendeleo vijijini, uvuvi na kilimo

FAO yakidhi kiu ya wafugaji na wakulima huko Togo

Ukuaji wa Kiuchumi

Maji ni hai ni kauli ambayo imethibitika kwa wakazi wa jimbo la Dankpen nchini Togo, baada ya Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la chakula na kilimo, FAO na serikali, kukarabati bwawa linalotumika hivi sasa kwa shughuli siyo tu za umwagiliaji, bali pia maji kwa wanyama na utalii.

Bustani ya mboga imeshamiri katika mkoa wa Dankpen nchini Togo, umwagiliaji ukiendelea, na maji yakichotwa kutoka bwawa la Gbangbale lililokarabatiwa na FAO.

Bwana hili ambalo historia yake ni tangu zama za ukoloni, liliharibika na kushindwa kushikilia maji na hivyo kutishia upatikanaji wa chakula kupitia umwagiliaji, mifugo na hata ujio wa watalii wanaofika hapa kutazama mamba na viumbe vingine hai.

Mamba hao pia wana umuhimu mkubwa katika mila na tamaduni za watu wa kabila la Konkoumba mkoani Dankpen.

Arouna Thcheou ni mfugaji na anasema bwawa hili litanufaisha wananchi, kwa sababu wakati wa ukame, ng’ombe wanafika hapa kunywa maji.

Ziara ya ukaguzi imefanyika ambapo FAO na mamlaka za mkoa wa Dankpen wanathibtisha kuwa mradi umetekelezwa vyema.

Mwakilishi Msaidizi wa FAO nchini Togo, Oyetounde Djiwa anasema waliitikia wito wa serikali wa kusaidia ukarabati wa bwawa ili liwe na uwezo wa kushikilia maji na gharama ilikuwa zaidi ya dola laki 9.

Bwana Djiwa anasema «Kuhusu masuala ya bayonuai, kwetu sisi ilikuwa ni muhimu kuhifadhi makazi haya ya mamba. Na ili kulinda mazingira kwenye eneo hili, unaweza kuona pia tulipanda pia miti ili kurejesha ile iliyokatwa wakati wa ujenzi wa bwawa. Kwa hiyo kwetu sisi pamoja na kuruhusu wafugaji kuendelea kunywesha mifugo yao hapa, wakulima kumwagilia mboga za majani, na kutunza bayonuai ilikuwa ndio kichocheo chetu. »

Sasa usimamizi wa bwawa hili uko mikononi mwa mamlaka za mkoa ambapo Soradjidine Ibriga, Naibu Meya wa Dankpen anasema « lazima tusimamie uendeshaji wake, na mkutano wa manispaa utapanga mipango ili hatimaye kila mwananchi anufaike na uwepo wa bwawa hili. »