Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Angola badili sheria ya kuengua watu wenye ulemavu kusimamia haki zao- UN

Moses Njoroge na David Gathu  kutoka Kenya wametumia teknolojia za kujifunza wenyewe na kutengeneza roboti ya kusaidia watu wenye ulemavu.
UN/Jason Nyakundi
Moses Njoroge na David Gathu kutoka Kenya wametumia teknolojia za kujifunza wenyewe na kutengeneza roboti ya kusaidia watu wenye ulemavu.

Angola badili sheria ya kuengua watu wenye ulemavu kusimamia haki zao- UN

Haki za binadamu

Nchini Angola watu wenye ulemavu hawana haki ya usimamizi wa fedha zao au kuingia mikataba, jambo ambalo limetia hofu Kamati ya Umoja wa Mataifa ya usimamizi wa mkataba wa haki za watu wenye ulemavu, CRPD.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za binadamu, imesema kamati hiyo imekutana leo Geneva, Uswisi na kupitia taarifa za mataifa 6 ikiwemo Angola kuhusu utekelezaji wao wa mkataba huo wa haki za watu wenye ulemavu, CRPD.

Kilichotia hofu zaidi kamati hiyo ni kwamba nchini Angola haki ya mtu mwenye ulemavu ya kufanya uamuzi kama vile usimamizi wa fedha na mali, mikataba ya kisheria na masuala ya afya bado anapatiwa mtu mwingine, jambo ambalo linamnyima haki mtu mwenye ulemavu kwa kisingizio cha ulemavu wa akili au kisaikolojia.

Kamati imetaka Angola ihakikishie watu wenye ulemavu haki sawa ya kutambuliwa mbele ya sheria na wakati huo huo iweke mfumo wa kusaidia utoaji wa maamuzi ya watu hao wenye ulemavu wakati wote wa uhai wao.

Changamoto nyingine iliyobainika ni ajira kwa watu wenye ulemavu ambapo licha ya amri ya Rais ya kwamba asilimia ya waajiriwa wenye ulemavu kwenye sekta ya umma isipingue asilimia 4 na sekta binafsi asilimia 2, takwimu za sasa zinaonesha kiwango hicho hakijafikiwa.

Kamati imeitaka Angola isimamie utekelezaji wa amri hiyo katika sekta zote za umma na binafsi, mathalani kwa kuweka adhabu kwa wale ambao hawatozingatia.

Nchi zingine ambazo zimefanyiwa mapitio ni Argentina, Georgia, Peru, Togo na Tunisia.

Huko Peru, kilichotia hofu kamati ni mipango ya serikali ya kujenga vituo zaidi vya makazi ambavyo vitakuwa kama taasisi mahsusi kwa watu wazima na watoto wenye ulemavu.

Kwa upande wa Georgia, mashirika yanayoendeshwa na watu wenye ulemavu hayapati ufadhili wa fedha kutoka serikalini na hivyo kutegemea zaidi misaada kutoka mashirika ya kimataifa ili kusongesha harakati zao za uchechemuzi.

Kamati imeitaka Georgia ihakikishe uhuru wa watu wenye ulemavu kujiunga kwenye vikundi ikiwemo kuwapatia hakikisho la kupata ufadhili wa kitaifa na vile vile fedha kutoka nje zinakuwa ni halali.

Tathmini ya Togo imetia wasiwasi kamati baada ya kubainika kutokuweko kwa mifumo inayozuia ubaguzi kwa misingi ya ulemavu, na watu hao kunyimwa malazi yanayofaa.

Kamati imeitaka Togo iweke mikakati ya kisheria ya kutambua kuwa kumnyima malazi mtu kwa msingi wa ulemavu ni ubaguzi.

Ripoti kamili inapatikana hapa.