Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanasiasa DRC malizeni tofauti zenu kwa mazungumzo- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Matafa António Guterres
UNFCCC Secretariat/James Dowson
Katibu Mkuu wa Umoja wa Matafa António Guterres

Wanasiasa DRC malizeni tofauti zenu kwa mazungumzo- Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani matukio ya ghasia yaliyofanyika katika siku mbili zilizopita ndani na nje ya jengo la bunge kwenye mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

 

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa ghasia hizo zimetokea jumatatu na jumanne ambapo baadhi ya mawaziri walipindua meza na kurushiana vitai baada ya hatua ya Rais Felix Tshisekedi kuvunja uongozi wa kishirika.

Mapema Jumapili Rais Tshisekedi alitangaza mpango wake wa kuunda ushirika mpya wa kiserikali wakati ushirika wa sasa una mawaziri ambao wanatoka chama cha FCC cha Rais wa zamani Joseph Kabila Ghasia wana wabunge 300 kati ya 500 kwenye bunge hilo.

Alinukuliwa akisema kuwa anaweza kuvunja bunge na kuitisha uchaguzi mpya iwapo hataweza kuunda serikali mpya ya ushirikiano.

Vuta nikuvute hiyo ilizua ghasia hizo ambapo Katibu Mkuu Guterres kupitia taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake jijini New York Marekani amesihi wanasiasa wamalize tofauti zao kwa amani, kupitia mashauriano kwa mujibi wa katiba na kwa maslahi ya wananchi wa DR Congo.

Bwana Guterres amerejelea msimamo wa Umoja wa Mataifa wa kuendelea kusaidia serikali ya DRC na watu wake katika juhudi zao za kujenga taasisi thabiti, zinazofanya kazi na kushughulikia changamoto za kiusalama, kiafya, kiuchumi na kijamii zinazokabili nchi hiyo ya Maziwa Makuu kwa muda mrefu sasa.

Vyombo vya habari vinasema kuwa Rais Tshisekedi ambaye ameingia madaraknai mwaka 2019 anahitaji kuunda serikali ya ushirika kati ya chama chake cha CaCH kile cha FCC ambacho kinadaiwa kuzuia marekebisho makubwa yanayohitajika.

Marekebisho hayo ni pamoja na usalama wa taifa, usimamizi wa rasilimali za nchi, uhuru wa mahakama na usimamizi wa chaguzi.

Bunge limeripoti kusitisha kikao hadi tarehe nyingine itakayopangwa kwa kile inachosema ni kuharibiwa kwa samani za bunge na uwepo wa walinzi wenye silaha ndani ya ukumbi wa bunge.
TAGS: DRC, Bunge