Idadi ya watu wanaohama kwa kulazimishwa yavuka milioni 80, COVID-19 nayo ikizidisha machungu

Wakimbizi kutoka Côte d’Ivoire wakisubiri kuandikishwa huko Liberia Oktoba 2020.
© UNHCR/Roland Tuley
Wakimbizi kutoka Côte d’Ivoire wakisubiri kuandikishwa huko Liberia Oktoba 2020.

Idadi ya watu wanaohama kwa kulazimishwa yavuka milioni 80, COVID-19 nayo ikizidisha machungu

Wahamiaji na Wakimbizi

Wakati picha kamili ya mwaka 2020 bado haijafahamika, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, linakadiria kuwa uhamishaji wa kulazimishwa ulimwenguni au ufurushwaji ulizidi milioni 80 katikati ya mwaka, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa hii leo mjini Geneva Uswisi kuhusu mwenendo wa uhamishaji wa kulazimishwa ulimwenguni.  

Mwanzoni mwa mwaka huu wa 2020, watu wengine milioni 79.5 walikuwa wamelazimishwa kutoka nyumbani kwao kwa sababu ya mateso, mizozo, na ukiukaji wa haki za binadamu. Jumla hii ilijumuisha wakimbizi wa ndani milioni 45.7, wakimbizi milioni 29.6 na wengine waliohamishwa kwa nguvu nje ya nchi yao, na wasaka hifadhi milioni 4.2. Migogoro iliyopo na ile mipya na pia virusi vya corona vimeathiri maisha ya watu hawa katika mwaka huu.  

Licha ya wito wa haraka wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres mwezi Machi wa kusitisha vita duniani wakati ulimwengu unapambana na janga la corona, mizozo na mateso vimeendelea. Vurugu nchini Syria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Msumbiji, Somalia, na Yemen zilishuhudia ufurushwaji mpya katika nusu yam waka 2020. Ufurushwaji mpya mkubwa umerekodiwa pia kote katika eneo la Sahel ya Kati barani Afrika, raia wakikabiliwa na vurugu za kikatili, pamoja na ubakaji na Makazi yao makubwa pia yamesajiliwa katika eneo lote la Sahel ya Kati wakati raia wanakabiliwa na vurugu za kikatili, pamoja na ubakaji na kuuawa. 

"Kuhama kwa kulazimishwa kukiongezeka maradufu katika muongo mmoja uliopita, jamii ya kimataifa inashindwa kulinda amani. Sasa tunapita hatua nyingine mbaya ambayo itaendelea kukua isipokuwa viongozi wa ulimwengu wakiacha vita." Amesema Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa UNHCR.  

Wakimbizi kutoka Ethiopia wakijiandikisha na UNHCR katika kambi ya Um Rakuba Al Qadarif, Sudan baada ya kukimbia makwao.
© UNHCR/Will Swanson
Wakimbizi kutoka Ethiopia wakijiandikisha na UNHCR katika kambi ya Um Rakuba Al Qadarif, Sudan baada ya kukimbia makwao.

Mzigo wa COVID-19 

UNHCR inasema, kwa watu waliolazimika kukimbia, COVID-19 imekuwa shida ya ziada juu ya dharura ya afya ya umma duniani. Virusi vimevuruga kila nyanja ya maisha ya binadamu na kuzidisha sana changamoto zilizopo kwa waliohama kwa nguvu na wasio na utaifa. 

Baadhi ya hatua za kuzuia kuenea kwa COVID-19 zilifanya iwe ngumu kwa wakimbizi kufikia usalama. Katika kilele cha wimbi la kwanza la janga hilo mnamo Aprili, nchi 168 zilifunga mipaka yao kikamilifu au kwa sehemu, na nchi 90 hazikutoa nafasi angalau ya upendeleo kwa wanaotafuta hifadhi. Tangu wakati huo, na kwa msaada na utaalam wa UNHCR, nchi 111 zimepata suluhisho za kiutendaji kuhakikisha mfumo wao wa hifadhi unafanya kazi kikamilifu au kwa sehemu wakati kuhakikisha hatua muhimu zinachukuliwa kuzuia kuenea kwa virusi. 

Licha ya hatua hizo, maombi mapya ya ukimbizi yalipungua kwa theluthi moja ikilinganishwa na kipindi kama hicho mnamo 2019. Wakati huo huo, sababu za msingi zinazosababisha mizozo ulimwenguni bado hazijashughulikiwa. 

Suluhisho chache za kudumu zimepatikana kwa waliohamishwa mwaka huu 2020 ikilinganishwa na kipindi kama hicho katika miaka iliyopita. Watu 822,600 tu waliokimbia makazi yao walirudi nyumbani, wengi kufikia 635,000 walikuwa wakimbizi wa ndani. Pamoja na kurudishwa kwa hiari kwa watu 102,600 katika nusu ya kwanza ya mwaka, urejeaji wa wakimbizi umeshuka kwa asilimia 22 ikilinganishwa na mwaka 2019. 

Kusafiri kwa wakimbizi kwenda katika nchi nyingine kupata makazi mapya kulisimama kwa muda kutokana na vizuizi vya COVID-19 kutoka Machi hadi Juni. Kwa hivyo, ni wakimbizi 17,400 tu waliopewa makazi yao katika miezi sita ya kwanza ya 2020 kulingana na takwimu za serikali, nusu ya takwimu ya 2019. 

 “Ingawa idadi halisi ya watu wasio na utaifa bado haijulikani, nchi 79 ulimwenguni zimeripoti kuwa na watu milioni 4.2 wasio na utaifa katika eneo lao.” Imeeleza taarifa ya UNHCR.