Wahamiaji wengi wazidi kupoteza maisha wakikimbilia Ulaya kupitia visiwa vya Canary- IOM 

20 Novemba 2020

Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM limeeleza wasiwasi mkubwa juu ya ongezeko la vifo vya wahamiaji vinavyotokea wakati wakisafiri kutoka pwani za Afrika kueleka visiwa vya Canary barani Ulaya. 

Taarifa ya IOM iliyotolewa leo mjini Dakar, Senegal inasema kuwa mwaka huu pekee mradi wa shirika hilo wa kufuatilia wahamiaji waliopotea umerekodi zaidi ya vifo 500 na idadi kubwa ni katika mwezi uliopita wa Oktoba na huu wa Novemba. 

“Kuna ongezeko kubwa la watu wanaoondoka kupitia pwani za nchi za Afrika Magharibi ikiwemo Senegal. Idadi ya vifo mwaka huu tayari ni maradufu ya vifo vilivyoripotiwa mwaka 2019 ambapo IOM ilisajili vifo 210 pekee kwa mwaka mzima kwenye eneo hilo, “ imesema taarifa ya IOM. 

Hata hivyo IOM inasema idadi hiyo ya mwaka huu ni kiwango cha chini na kuna hofu kuwa idadi inaweza kuwa kubwa zaidi. 

Mkurugenzi wa IOM wa uchambuzi wa takwimu duniani, Frank Laczko amesema shirika lao linakabiliwa na changamoto nyingi katika kukusanya takwimu kwenye njia ya Afrika Magharibi, hasa pale wanapopokea ripoti kuhusu kutoweka kwa boti bila kuwa na uwezo wa kuifuatilia. 

Amemulika tukio la hivi karibuni la boti kuzama karibu na pwani ya Cabo Verde, ambako wahamiaji 66, wakiwemo watoto, waliwasili wakiwa kwenye boti iliyoharibika. 

Bwana Lackzo amesema kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya serikali pamoja na manusura hao, zaidi ya watu 130 walipanda kwenye chombo hicho kabla ya injini yake kulipuka. 

“Watu 60 yasadikiwa walipoteza maisha kwenye tukio hilo la mlipuko. Takribani wote waliokuwemo kwenye boti hiyo walikuwa raia wa Senegal isipokuwa watu wawili tu kutoka Gambia,”  alisema afisa huyo wa IOM. 

Kwa sasa IOM inashirikiana na wadau wa eneo hilo na jamii ili kuthibitisha ripoti na takwimu kuhusu majanga kama hayo. 

Shirika hilo linasema takwimu za aina hiyo ni muhimu katika kuchangia kwenye sera nzuri na bora za uhamiaji unaojali utu sambamba na mahitaji ya usimamizi wa uhamiaji. 

Hadi mwaka huu wa 2020, wahamiaji 18,000 wamewasili visiwa vya Canary huko Hispania baada ya safari ndefu na hatari kuvuka bahari ya Atlantic. 

Takribani 12,000 kati yao waliwasili mwezi Oktoba na Novemba mwaka huu na wengi wao wanatoka nchi za Afrika Magharibi. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter