Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya sasa ya wagonjwa wa Ebola DR Congo imeongezeka kuliko mlipuko uliopita-WHO

Katika kliniki moja  ya kutibu wagonjwa wa Ebola huko Mbandaka jimbo la Kivu Kaskazini, mhudumu akiwa amevalia mavazi rasmi ili kuepusha maambukizi.
Shirikisho la vyama vya msalaba mwekundu na hilal nyekundu
Katika kliniki moja ya kutibu wagonjwa wa Ebola huko Mbandaka jimbo la Kivu Kaskazini, mhudumu akiwa amevalia mavazi rasmi ili kuepusha maambukizi.

Idadi ya sasa ya wagonjwa wa Ebola DR Congo imeongezeka kuliko mlipuko uliopita-WHO

Afya

Mlipuko wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC katika jimbo la Equateur unaendelea kuongezeka na kusababisha wasiwasi kwa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa WHO na wadau wake ambao kwa sasa wanakabiliwa na pengo la ufadhili, imesema taarifa iliyotolewa na WHO kanda ya Afrika mjini Brazzaville, Jamhuri ya Congo.

Taarifa hiyo ya WHO imeeleza kuwa idadi ya wagonjwa wa mlipuko wa sasa imeizidi ile ya wagonjwa waliorekodiwa katika mlipuko wa mwisho uliotokea mwaka 2018.

Mlipuko huu mpya wa sasa ambao ni wa 11 nchini DRC, ulitangazwa tarehe mosi ya mwezi Juni mwaka huu wa 2020 baada ya wagonjwa kugundulika katika maeneo ya Mbandaka katika jimbo la Equateur.

WHO inasema mlipuko wa ugonjwa, tangu wakati huo umesambaa katika kanda tano za kiafya, kukiwa na wagonjwa 56 waliorekodiwa. Mji wa Mbandaka na viunga vyake vilikuwa kitovu cha mlipuko wa 9 wa Ebola ambao ulidumu kuanzia mwezi Mei hadi Julai mwaka 2018 ambapo wagonjwa 54 walithibitika.

“Katika wagonjwa 56 ambao wameripotiwa hadi kufikia hivi sasa, 53 wamethibitika kuwa na maambukizi, na watatu wana uwezekano wa kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo. Katika wiki tatu pekee, wagonjw28 wamethibitika.” WHO imeeleza.

Dkt Matshidiso Moeti, amabye ni Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika amesema, “kukabiliana na Ebola katikati ya janga la COVID-19 linaloendelea, ni vigumu lakini hatutakiwi kuiacha COVID-19 ituzuie kupambana na vitishpo vingine vya kiafya.”

Hata hivyo WHO inaeleza kuwa mapambano ya sasa dhidi ya Ebola yanakabiliwa na changamoto za ufadhili. Hadi kufikia sasa WHO imekusanya dola milioni 1.5 za kimarekani ambazo zitadumu kwa wiki chache zijazo. Shirika hilo la afya la Umoja wa Mataifa limekuwa likijitahidi kwa kushirikiana na Wizara ya Afya ya DRC na wadau kukuza ufahamu katika jamii kuhusiana na ugonjwa  na kutaka uungwaji mkono kutoka katika jamii. Kaya 40,000 zimetembelewa nan a wahudumu wa afya na zaidi ya watu 273,00 wamepewa taarifa za kiafya na usalama.

TAGS: Ebola, WHO, DRC