Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlipuko wa karibuni wa Ebola wakunja jamvi DRC: WHO

Mhudumu wa afya akimchanja dhidi ya Ebola, mwanaume mjini Beni, mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC.
World Bank/Vincent Tremeau
Mhudumu wa afya akimchanja dhidi ya Ebola, mwanaume mjini Beni, mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC.

Mlipuko wa karibuni wa Ebola wakunja jamvi DRC: WHO

Afya

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO leo limetangaza kwamba mlipuko wa Ebola uliozuka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kwenye jimbo la Kivu ya Kaskazini mwezi Oktoba ukiwa ni wa pili kwa mwaka 2021 sasa umemalizika. 

Tangazo la kumalizika kwa mlipuko huo limetolewa na mamlaka ya kitaifa ya afya nchini DRC baada ya kutokuwa na mgonjwa yeyote mpya aliyeripotiwa mwishoni mwa siku 42 za kuangalia na kufuatilia ugonjwa huo, au vitindi viwili vya kusubiria tangu kuliporipotiwa mgonjwa wa mwisho na kuruhusiwa kwenda nyumbani. 

Jumla ya wagonjwa walioambukizwa 

Kwa jumla, kulikuwa na wagonjwa 11 na wanane walithibitishwa, huku watatu wakishukiwa,  ikijumuisha pia vifo sita viliripotiwa katika mlipuko huo uliotangazwa rasmi tarehe 8 Oktoba baada ya kisa kipya kuthibitishwa katika eneo la afya la Beni kwenye mkoa wa Kivu Kaskazini nchini humo.

WHO inasema huu ulikuwa mlipuko wa 13 wa nchi hiyo na ulitokea katika eneo sawa na mlipuko wa 2018 ambao ulidumu  kwa miaka miwili. 

Zaidi ya watu 1800 walichanjwa katika kampeni iliyoanza siku tano tu baada ya mgonjwa wa kwanza kugunduliwa.  

Mlipuko huo unaadhimisha mara ya kwanza ya matumizi ya chanjo ya ERVEBO iliyoidhinishwa hivi majuzi kutumika dhidi ya Ebola nchini humo.  

ERVEBO ni sawa na matumizi ya chanjo ya huruma, lakini ni chanjo iliyoidhinishwa, na utoaji wa chanjo hiyo hauana changamoto kubwa. 

"Ufuatiliaji thabiti wa magonjwa, ushirikishwaji wa jamii, chanjo inayolengwa na hatua za haraka vinafanywa ili kudhibiti Ebola katika eneo hili," amesema Dkt. Matshidiso Moeti, mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika.  
Ameongeza kuwa "Wakati wa mlipuko huu, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo iliweza kupunguza maambukizi, kusambaa kwa mlipuko huo na kuokoa maisha. Kuna mengi tuliyojifunza na tunayatumia masomo hayo katika kila mlipuko unaozuka.”  

Hatua Madhubuti na za haraka zinaojumuisha mikakati muhimu ya kudhibiti milipuko kama vile ufuatiliaji wa watu walio karibu na mgonjwa, upimaji, ufuatiliaji wa magonjwa na juhudi za ushirikiano wa jamii zilisaidia kudhibiti mlipuko huo ndani ya mji wa Beni, ambako kisa cha kwanza kiligunduliwa.

Katika kuunga mkono nchi, WHO ilipeleka wataalam, vifaa, na pesa zilizochangia kusaidia kudhibiti milipuko huo. 

Hata hivyo, usalama usiotabirika na wakati mwingine hali tete katika sehemu za Beni vilitatiza hatua za kupambana na mlipuko huo katika baadhi ya maeneo, huku wahudumu wa afya na wahudumu wengine wa mstari wa mbele wakishindwa kufikia maeneo yasiyo na usalama kufuatilia watu walio katika hatari kubwa au kutoa chanjo. 

Jinsi chanjo ya ebola inavyopatiwa binadamu ili kumkinga na ugonjwa huo. Pichani ni wakati wa mlipuko huko Equateur ambapo Dkt. Alhassane Toure anampatia chanjo mhudumu wa afya katika kituo cha Mbandaka, nchini DRC
WHO/Lindsay Mackenzie
Jinsi chanjo ya ebola inavyopatiwa binadamu ili kumkinga na ugonjwa huo. Pichani ni wakati wa mlipuko huko Equateur ambapo Dkt. Alhassane Toure anampatia chanjo mhudumu wa afya katika kituo cha Mbandaka, nchini DRC

Kuzuia ukatili wa kingono kumesaidia pia 

Kuzuia unyanyasaji wa kijinsia na ukatili wa kingono kulikuwa nguzo kuu ya hatua za kupambana na Ebola 
Mtaalamu alitumwa kutoa mafunzo kwa wafanyikazi na washirika wa WHO juu ya kuzuia tabia isiyofaa na ya kikatili. 

Kila mtu anayehusika katika kazi za mashinani alipata mafunzo na kila wakala mshirika alitia saini kanuni za maadili.  

Wakufunzi walishirikiana moja kwa moja na wanajamii ambapo mamlaka za afya zilikuwa zikifanya kazi ili kuongeza ufahamu kuhusu unyanyasaji na ukatili wa kingono na jinsi ya kuripoti kwa usalama.  

Matangazo ya redio na vipeperushi katika lugha za kienyeji pia yalisaidia kueneza ujumbe. 

Huku mlipuko huo ukitangazwa kuwa umemalizika, mamlaka za afya zinaendelea na ufuatiliaji na ziko tayari kuchukua hatua haraka endapo milipuko yoyote mipya itazuka.  

Kwa mujibu wa WHO sio kawaida kwa visa vya hapa na pale kutokea kufuatia mlipuko mkubwa.  
Matokeo ya mfuatano wa jeni yaliyofanywa na taasisi ya kitaifa ya utafiti wa tiba ya kibiolojia nchini humo yamegundua kuwa kisa cha kwanza cha Ebola kilichogunduliwa katika mlipuko uliokwisha kumalizika huenda kiliwakilisha mwanzo mpya wa mlipuko wa Ebola wa 2018-2020 kutokana na kuendelea kuwepo kwa virusi hivyo katika jamii. 

Nchi hiyo imeanzisha mpango wa waathirika wa Ebola ambao kwa sasa una zaidi ya watu 1,100 kutokana na milipuko ya awali katika mkoa wa Kivu Kaskazini.  

Watu wawili walionusurika kutokana na mlipuko uliomalizika wamesajiliwa katika mpango wa manusura.

Kwa muda wa miezi 18 ijayo watapata uchunguzi wa kila mwezi, ambao unajumuisha tathmini za matibabu, msaada wa kisaikolojia na lishe.