Mwongozo mpya wa WHO kusaidia utambuzi wa haraka wa viwango vya madini ya chuma mwilini

21 Aprili 2020

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, limetoa mwongozo mpya wa kuweza kusaidia kubaini mapema ukosefu wa madini ya chuma mwili sambamba na uwepo wa madini mengi ya aina hiyo kupita kiasi mwilini.
 

WHO inasema mwongozo huo wa kipimo cha kiwango cha kemikali aina ya Ferritin ili kutathmni hali ya madini ya chuma mwilini, utasaidia wahudumu wa afya kutambua mapema ukosefu wa madini ya chuma na hivyo kuepusha madhara makubwa zaidi.
Ferritin ni aina ya protini inayopatikana kwa kiasi kidogo katika damu ya binadamu ambapo iwapo mtu akipimwa akiwa na kiwango cha chini ina maana kiwango cha madini ya chuma ni kidogo na iwapo protini hiyo ipo kwa kiwango cha juu, basi madini ya chuma nayo yapo kwa kiwango cha juu kupita kiasi.
WHO inasema kuwa kiwango kidogo cha madini ya chuma kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 2 kinaweza kuwa na madhara yasiyotibika kwenye maendeleo ya ubongo wao na hatimaye kukwamisha uwezo wao wa kujifunza shuleni.
Kwa watu wazima, ukosefu wa madini ya chuma unasababisha uchovu, ukosefu wa tija kazini na hata ukosefu wa damu mwilini.

Mama na mwanae mchanga wakipata huduma baada ya kujifungua kwenye wodi ya wazazi iliyoko kliniki ya Shakawe nchini Botswana.
UNICEF/Christine Nesbitt
Mama na mwanae mchanga wakipata huduma baada ya kujifungua kwenye wodi ya wazazi iliyoko kliniki ya Shakawe nchini Botswana.

WHO inasema kuwa kwa upande wa kuwepo kwa kiwango cha juu cha madini ya chuma mwilini, nalo ni tatizo linaloweza kusababishwa na kurithi ambapo “kutoa damu mara kwa mara ili kupunguza kiwango cha madini hayo mwilini kinaweza pia kuzorotesha afya ya mhusika iwapo hatopatiwa tiba.”
WHO inakumbusha kuwa madini ya chuma ni muhimu sana mwilini hasa katika kusafirisha hewa ya oksijeni, uchambuzi wa vijinasaba na kuwezesha misuli kufanya kazi.
Akizungumzia mwongozo huo, Dkt. Francesco Branca, ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Lishe na Usalama wa Chakula, WHO, amesema kuwa kuimarisha uwezo wa kutambua kiwango cha ukosefu wa madini ya chuma na hatari ya madini hayo kuwepo kwa kiwango kikubwa mwilini kutasaidia nchi kuamua mipango ya afya kwa lengo la kufuatilia na kulinda wananchi wake.“Mathalani, ukosefu wa madini ya chuma utokanao na lishe dunia, unaweza kubainika pia miongoni mwa watu wenye maambukizi ya magonjwa. Tathmini ya kutosha ya hali ya madini ya chuma kwenye nchi zenye maambukizi kunaweza kusaidia nchi hizo kuandaa sera bora za afya,”  amesema Dkt. Branca.
 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter