Udhibiti wa COVID-19 usiingilie mnyororo wa usambazaji wa chakula-FAO, WHO, WTO

Umoja wa Mataifa na harakati za kusaidia kuhakikisha uhakika wa chakula.
IFAD/GMB Akash
Umoja wa Mataifa na harakati za kusaidia kuhakikisha uhakika wa chakula.

Udhibiti wa COVID-19 usiingilie mnyororo wa usambazaji wa chakula-FAO, WHO, WTO

Afya

Mashirika ya Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo duniani, FAO, la afya WHO na lile la biashara duniani yamesema mamilioni ya watu ulimwenguni kote hutegemea biashara ya kimataifa kwa uhakika wao wa chakula na riziki. Wakati nchi zinachukua hatua za kudhibiti janga la virusi vya corona, COVID-19, ni lazima kuwa makini ili kupunguza athari zinazoweza kupatikana katika usambazaji wa chakula au matokeo yasiyotarajiwa katika biashara ya kimataifa na usalama wa chakula.

Kupitia taarifa yao ya pamoja yamesema, wakati wa kulinda afya na ustawi wa raia wao, nchi zinapaswa kuhakikisha kuwa hatua zozote zinazohusiana na biashara haziingilii mnyororo wa usambazaji wa chakula. Rabsha kama hiyo ikiwa ni pamoja na kudhoofisha harakati za wafanyikazi wa tasnia ya kilimo na chakula na kupanua kucheleweshwa kwa vyombo vya chakula kwenye mipaka, kutasababisha uharibifu na kuongeza taka za chakula. Vizuizi vya biashara ya chakula pia vinaweza kuhusishwa na wasiwasi usio na msingi juu ya usalama wa chakula. Ikiwa hali kama hiyo itatokea, itaathiri msururu wa usambazaji wa chakula, na kuleta madhara makubwa kwa watu walio katika mazingira magumu zaidi wasiokuwa na uhakika wa chakula.

Kwa mujibu wa mashirika hayo, kutokuwa na uhakika juu ya upatikanaji wa chakula kunaweza kusababisha wimbi la vizuizi vya kuuza bidhaa nje, na kusababisha uhaba katika soko la kimataifa. Athari kama hizi zinaweza kubadilisha usawa kati ya usambazaji wa chakula na mahitaji, na kusababisha kuongezeka kwa bei na kuongezeka kwa hali mfumko wa bei. Taarifa hiyo imenukuu mashirika hayo yakisema, “tulijifunza kutoka kwa majanga ya awali kwamba hatua kama hizo zinaathiri sana nchi zenye mapato ya chini, upungufu wa chakula na kwa juhudi za mashirika ya kibinadamu kupata chakula kwa wale wanaohitaji msaada."

Lazima tuzuie kurudia kwa hatua kama hizo za uharibifu. Ni wakati kama huu ambapo ushirikiano wa kimataifa unakuwa muhimu. Katikati ya janga la COVID-19, kila juhudi lazima zifanywe ili kuhakikisha kuwa biashara inapita kwa uhuru iwezekanavyo, hususan katika kuzuia uhaba wa chakula. Vile vile, ni muhimu pia kwamba wazalishaji wa chakula na wafanyikazi wa chakula katika kiwango cha usindikaji na rejareja walindwe ili kupunguza ueneaji wa ugonjwa ndani ya sekta hii na kudumisha minyororo ya usambazaji wa chakula. Watumiaji, haswa walio hatarini zaidi, lazima waendelee kupata uwezo wa kupata chakula ndani ya jamii zao chini ya mazingira salama.

Lazima pia tuhakikishe kwamba taarifa juu ya hatua za biashara zinazohusiana na chakula, viwango vya uzalishaji wa chakula, matumizi na hifadhi, na pia bei ya chakula, inapatikana kwa wote kwa wakati halisi. Hii inapunguza kutokuwa na uhakika na inaruhusu wazalishaji, watumiaji na wafanyabiashara kufanya maamuzi sahihi. Zaidi ya yote, inasaidia kukabiliana na manunuzi kwa hofu na kushikilia bidhaa kwa malengo ya kusababisha uhaba sokoni chakula na bidhaa zingine muhimu.

Mashirika hayo yamesema, sasa ni wakati wa kuonesha mshikamano, na kuzingatia lengo letu la pamoja la kuhakikisha uhakika wa chakula, usalama wa chakula na lishe na kuboresha ustawi wa jumla wa watu kote ulimwenguni. Lazima tuhakikishe kuwa mwitikio wetu katika kukabiliana na COVID-19 hausababishi bila kukusudia uhaba wa vitu muhimu na kuzidisha njaa na utapiamlo.