Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 mbali ya afya inaathiri maisha na mifumo ya chakula:FAO /ILO/IFAD

Nchini Guaemala WFP ikisambaza chakula kwa jamii za asili ambao wameathirika na ukosefu wa uhakika wa chakula kufuatia athari za kijamii za COVID-19
WFP/Carlos Alonzo
Nchini Guaemala WFP ikisambaza chakula kwa jamii za asili ambao wameathirika na ukosefu wa uhakika wa chakula kufuatia athari za kijamii za COVID-19

COVID-19 mbali ya afya inaathiri maisha na mifumo ya chakula:FAO /ILO/IFAD

Masuala ya UM

Taarifa ya pamoja iliyotolewa na mashirika ya Umoja wa Mataifa imeonya kwamba hatua madhubuti zisipochukuliwa sasa kukabiliana na athari za janga la corona au COVID-19 kwa maisha ya watu, ajira na mifumo ya chakula basi uhakika wa chakula duniani utakuwa njiapanda

Katika taarifa hiyo ya pamoja ya shirika shirika la chakula na kilimo FAO, shirika la kazi duniani ILO na mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo IFAD, iliyotolewa leo mjini Roma Italia kuelekea siku ya chakula duniani itakayoadhimishwa Oktoba 16, yameitaka dunia kutafakari upya mustakabali wa mazingira , changamoto zake na kushughulikia changamoto ya mabadiliko ya tabianchi kwa haraka na kwa umakini. 

FAO imesema “Hadi pale hayo yatakapofanyika ndio tutaweza kulinda afya, maisha ya watu, mifumo ya chakula na lishe kwa watu wote na kuhakikisha kwamba kawaida yetu mpya inakuwa bora zaidi.” 

Shirika hilo limeongeza kuwa mamilioni ya biashara hivi sasa zinakabiliwa na tishio la kutoweka, karibu nusu ya watu wote wanaofanyakazi duniani ambao ni bilioni 3.3 wako hatarini kupoteza uwezo wao wakujikimu kimaiasha , huku wafanyakazi walio katika sekta zisizo rasmi wakiwa hatarini zaidi kwa kukosa ulinzi wa hifadhi ya jamii na fursa za huduma za afya na bila njia za kuweza kupata kipato. 

“Kwa wengi bila kipato inamaanisha hakuna mlo, au mlo mmoja, au lishe duni”limeonya shirika hilo na kuongeza kuwa hali hiyo itawafanya watu hawa kushindwa kulisha familia zao.

Kwa mujibu wa mashirika hayo janga la COVID-19 limeathiri vibaya mfumo mzima wa chakula kwani kufungwa kwa mipaka, vikwazo vya biashara na hatua za kusalia majumbani“vimewazuia wakulima kupata fursa za masoko, ikiwemo kununua pembejeo na kuuza mazao yao na wakulima kushindwa kuvuna mazao yao. Hali hiyo imeathiri mnyororo wa usambazaji wa chakula wa kitaifa na kimataifa na kupunguza fursa za upatikanaji wa vyakula bora, salama na mchanganyiko vinavyohitajika katika lishe.” 

Waathirika wakubwa mashirika hayo yamesema ni makundi ya walio wachache kama vile wakulima wadogowadogo na watu wa asili. 

Mashirika hayo yametoa wito kwa dunia nzima “kutambua fursa ya kujikwamua vyema kutoka kwenye janga hili kwa mshikamano na kuzisaidia hususan nchi zinazoendelea zisizojiweza, na kuweka mikakati endelevu kushughulikia changamoto za kiafya na za sekta ya kilimo na chakula zilizosababishwa na COVID-19, ili kuepuka janga kubwa zaidi siku za usoni.”