Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya wakimbizi 30,000 kutoka Sudan wasajiliwa Chad- UNHCR

Wanawake wakisubiri kusajiliwa na wafanyakazi wa UNHCR katika eneo la Koufroun katika eneo la Ouaddaï nchini Chad. Wote walikimbia mji wa Tindelti, mita mia chache kuvuka mpaka wa Sudan.
© UNHCR/Colin Delfosse
Wanawake wakisubiri kusajiliwa na wafanyakazi wa UNHCR katika eneo la Koufroun katika eneo la Ouaddaï nchini Chad. Wote walikimbia mji wa Tindelti, mita mia chache kuvuka mpaka wa Sudan.

Zaidi ya wakimbizi 30,000 kutoka Sudan wasajiliwa Chad- UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Nchini Chad, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limeanza kazi ya kusajili wakimbizi walioingia nchini humo kutoka Sudan kufuatia mapigano yanayoendelea kati ya jeshi la serikali na wanamgambo wa RSF kwenye mji mkuu wa taifa hilo Khartoum. Wakimbizi sasa pamoja na kusajiliwa wanapatiwa mahitaji muhimu. 

Kwenye mji huu wa Midjilita, jimboni Ouaddai, nchini Chad, ni ving’ora, purukushani za  hapa na pale huku wanawake wanaume na watoto wakipita huku na kule.

Ni harakati zenye ahueni miongoni mwa wakimbizi 30,000 kutoka Sudan ambao wameona nuru baada ya kufika hapa Midjilita, jimbo la OUADDAÏ nchini Chad.

Wakimbizi hawa wako hoi na miongoni mwao ni Raouda Abdallah Jaffar akiwa amebeba mtoto mmoja huku wengine wakiambatana naye! Wanajongea kwenye dawati la usajili lililoandaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR.

Baada ya usajili, Raoud anasema, “ nimesajiliwa leo na UNHCR. Nahitaji sasa matandiko, blanketi, chakula na mahitaji mengine.”

Usajili ukikamilika, wakimbizi wanaelekea sehemu ya kupatiwa vifaa muhimu kama alivyosema Raoud. Mmoja baada ya mwingine anapatiwa matandiko, vifaa vya jikoni na kadha wa kadha.

Huku wakimbizi wakisajiliwa na kupatiwa vifaa vya msaada, kwingineko hapa ujenzi unaendelea wa makazi ya wakimbizi sambamba na vyoo ili kuhakikisha huduma za kujisafi na usafi zinapatikana.

Jerome Sebastien Naibu Mwakilishi wa UNHCR nchini Chad anasema iwapo mzozo Sudan utaendelea kuna uwezekano wa Chad kupokea hadi wakimbizi 100,000 na mahitaji ya fedha kwa ajili ya kufanikisha operesheni za usaidizi yanaweza kufikia dola milioni 130.

Hivyo ametoa ombi kwa jamii ya kimataifa kusaidia Chad na mashirika ya kiutu yanayoshiriki katika harakati za kusaidia wakimbizi.

Amesema “ni wakati huu tunahitaji uhamasishaji wa fedha ili tuweze kuwahamishia wakimbizi hawa maeneo ya ndani zaidi kwa ajili ya usalama na pia wapate usaidizi makini.”