Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makazi ya wakimbizi: 'Pengo kubwa' linaendelea kati ya mahitaji, na nafasi zilizopo

Baba mzazi kutoka Syria anasimama na watoto wake katika kambi ya Bardarash mjini Duhok, Iraq, siku moja baada ya kuwasili.
UNHCR/Hossein Fatemi

Wahamiaji na Wakimbizi

Ingawa wakimbizi takribani milioni 1.4 duniani kote wanakadiriwa kuwa katika uhitaji wa haraka wa kupatiwa makazi mapya katika nchi nyingine, ni wakimbizi 63,696 pekee ambao walipata fursa hiyo kupitia shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR kwa mwaka jana 2019 hiyo ikiwa ni asilimia 4.5 pekee kutokana na kuendelea kwa upungufu wa serikali kote duniani kutoa nafasi hizo.

dadi ya kuwapatia makazi mapya wakimbizi katika mwaka 2019 iliongezeka kwa wastani wa asilimia 14 ikilinganishwa na mwaka uliopita yaani mwaka 2018 wakati watu 55,680 walipohamishishiwa katika nvchi nyingine na kupewa makazi, lakini UNHCR inasisitiza kwamba “pengo kubwa linabaki kati ya mahitaji na nafasi zilizopo.”

Makazi mapya ni hatua ya kuokoa maisha

Mkurugenzi wa ulinzi wa kimataifa wa UNHCR Grainne O’Hara anasema, “makazi mapya siyo sukuhisho kwa wakimbizi wote duniani lakini ni hatua ya kuokoa maisha kuhakikishia ulinzi wa wale ambao wako katika hatari na ambao maisha yao yanategemea huduma hiyo ya makazi mapya.”

Idadi kubwa ya wakimbizi waliopatiwa makazi mapya chini ya uratibu wa UNHCR mwaka jana walikuwa wanaelekea Marekani, ikifuatiwa na Canada, Uingereza, Sweden na Ujerumani.

Kati ya zaidi ya wakimbizi 63,000 ambao walipatiwa makazi mapya, idadi kubwa yao ilitoka Syria, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na Myanmar.

Kuongeza idadi ya nchi za kuwapokea wakimbizi

Mkimbizi kutoka Sudan mwenye umri wa miaka 26 anaishi katika Taratibu ya Udhibiti wa Dharura ya UNHCR nchini Niger, eneo salama kwa wakimbizi waliokoolewa kutoka kwenye hali mbaya katika vituo vya kufungwa nchini Libya.
UNHCR/Sylvain Cherkaoui
Mkimbizi kutoka Sudan mwenye umri wa miaka 26 anaishi katika Taratibu ya Udhibiti wa Dharura ya UNHCR nchini Niger, eneo salama kwa wakimbizi waliokoolewa kutoka kwenye hali mbaya katika vituo vya kufungwa nchini Libya.

Wakati lengo la mkakati la wakimbizi 60,000 kupatiwa makazi katika mataifa 29 tofauti lilifikiwa mwaka jana, UNHCR imesema ilikuwa na wasiwasi kwa kuzingatia makadirio ya sasa, wakimbizi wachache watafanikiwa kupatiwa makazi mapya mwaka huu. Mwaka huu, lengo ni nchi 31 kuwapa makazi wakimbizi 31,000 ambao wataidhinishwa na UNHCR.