Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Siku ya wakimbizi duniani

Mataifa yaliyoendelea toeni fursa zaidi kwa wakimbizi.

UN Photo/Eskinder Debebe
Siku ya wakimbizi duniani

Mataifa yaliyoendelea toeni fursa zaidi kwa wakimbizi.

Wahamiaji na Wakimbizi

Kuelekea siku ya wakimbizi duniani tarehe 20 juni, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameyahimiza mataifa yaliyoendelea duniani kutoa fursa zaidi kwa wakimbizi wanaosaka makazi mapya.

Gutteres ameyasema hayo alipowatembelea wakimbizi kutoka nchini Iraq na Afghanistan wanaoishi jijini New York Marekani. "Kama mamilioni ya wakimbizi duniani kote, wanasaidia kuleta maisha mapya, ustawi na utofauti tajiri kwa jumuiya zinazowapokea. Ni lazima tuendelee kuwaunga mkono,” mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alisema kwenye akaunti yake ya Twitter kufuatia ziara hiyo. Guterres, ambaye alikuwa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Wakimbizi kuanzia mwaka 2005 hadi 2015, alisisitiza nafasi muhimu ya mataifa yaliyoendelea katika kupokea wakimbizi na kuwapa fursa, yeyote yule na popote anapotoka. ‘Sitakufa kesho’ Ziara ya Kutembelea wakimbizi jijini New York ilianzia Brooklyn, ambapo alimtembelea Suzan Al Shammari, mkimbizi raia wa Iraqi ambaye mwaka 2010 alikimbia na familia yake kutoka Baghdad hadi Cairo, Misri. Walisajiliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, na waliweza kuhamishiwa tena California nchini Marekani. Kutoka huko, na kwa usaidizi zaidi, waliweza kusafiri hadi jijini New York. Bi Al Shammari alimweleza Katibu Mkuu kuwa kwa sababu alikulia vitani, anataka kuwa na uwezo wa kuwasaidia wakimbizi wengine. Nikutokana na sababu hiyo, kwa sasa anafanya kazi kama mfanyakazi katika shirika lisilo la kiserikali (NGO) baada ya hivi karibuni kuhitimu shahada ya uzamili katika chuo kikuu nchini Uingereza. "Kila siku unafikiri itakuwa ndio siku ya mwisho. Nilipoenda Misri pamoja na familia yangu ilikuwa vigumu pia kuwa huko kama mkimbizi katika hali ngumu. Kwa hivyo, kuhamia Marekani, ilikuwa baraka kubwa, ilinichukua miaka kadhaa kuzoea kwamba sitakufa kesho,” alisema Al Shammari. Aliongeza kuwa kuhamishwa kwenda nchi nyingine kunatoa fursa ya "nafasi ya pili" kwa wale wanaolazimika kuzikimbia nchi zao. “Kuleta wakimbizi ni hatua ya kuokoa maisha na ni jambo ambalo kila kiongozi, kila nchi, inapaswa kuchangia na kuwajibika kwa sababu ya madhila mengi yanayowakumba wakimbizi. Ni hatua ya kuokoa maisha kuchukua hatua hiyo na kupokea wakimbizi,” alisema Al Shammari. [scald=251332:sdl_editor_representation] Nina furaha ya kuhamia nchi ya tatu lakini wasiwasi kwa familia yao. Baada ya kukutana na Bi. Al Shammari, Katibu Mkuu Guterres alikwenda eneo la Queens kuwatembelea wanandoa kutoka Afghanistan, Shafi Alif na Rohina Sofizada. Akiwa katika nyumba yao, alikaribishwa kwa chai ya kijani iliyotiwa viungo na chipsi za kitamaduni za Kiafghani. Walipokuwa wakizungumza juu ya vikombe vyao, Alif alimueleza kwamba familia yake ilikimbia Afghanistan hadi Pakistani alipokuwa na umri wa miezi mitano, mwaka wa 1992. Familia hiyo ilitembea kwa siku 40 kutafuta hifadhi nchini Pakistani, ambako walikaa kwa zaidi ya miaka 10. Pia walisajiliwa na UNHCR. Kwa usaidizi wa UNHCR, Bw. Alif na familia yake walirejea Afghanistan kwa hiari mwaka 2002. Alipata usaidizi wa kifedha walipokuwa wakitua Kabul, ikiwa ni pamoja na usafiri, na posho ya pesa taslimu, miongoni mwa usaidizi mwingine. Wenza hao walikubali kuwa walikuwa na "miaka ya amani" nchini humo hadi 2018, wakati Bi Sofizada, ambaye alikuwa akifanya kazi na Ubalozi wa Marekani huko Kabul, alipokea visa maalum ya kuishi tena Marekani. Baadaye kidogo, Bwana Alif alijiunga naye kwa Visa Maalum ya Wahamiaji, alipokuwa akifanya kazi na Jeshi la Poland katika mji mkuu wa Afghanistan. Leo wana furaha kwamba wanaweza kufika Marekani, lakini bado wana wasiwasi kuhusu wanafamilia wao, ambao sasa wako Pakistan, baada ya kuondoka Kabul baada ya Taliban kushukua madaraka mwaka jana 2021. "Familia yangu ilikataliwa kwenye mpaka mara mbili, ijapokuwa walikuwa na visa na hati zote. Ilibidi watembee mpaka Pakistan kwa miguu, kwani pale walikuwa hawapokei Waafghani wengi. Tumefarijika kuwa hapa, lakini bado tunahangaikia jamaa zetu,” akasema Bi Sofizada. Kama vile Bi. Al Shammari, Bw. Shafi pia anafanya kazi kuwasaidia wageni. Yeye ni mfanyakazi wa kesi zisizo za kiserikali anayesaidia wahamishwaji na walioachiliwa huru kutoka Afghanistan wanaowasili. Anasema kuwa hakuna mkimbizi "aliye na furaha kuondoka katika nchi zao", lakini kwa sababu wamekuwa wakikabiliana na ghasia au mateso, wameamua kuondoka kwa sababu hawana chaguo jingine. "Tunahitaji maeneo zaidi ya makazi mapya, tunahitaji msaada zaidi kwa njia tofauti, kama vile mahitaji ya kimsingi, makazi, chochote ambacho ni muhimu kwa mkimbizi. Hivyo, wanaweza kuwa msaada kwa jamii wanayoishi,” alieleza. Kwa mujibu wa UNHCR, Waafghan ni miongoni mwa idadi kubwa ya wakimbizi duniani kote. Kuna wakimbizi milioni 2.6 waliosajiliwa kutoka Afghanistan kote ulimwenguni, kati yao milioni 2.2 wamesajiliwa nchini Iran na Pakistan pekee. Watu wengine milioni 3.5 ni wakimbizi wa ndani. Zaidi ya nusu ya idadi ya watu wa Afghanistan, au watu milioni 24, wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na asilimia 97 ya wakazi wa Afghanistan wanakadiriwa kuishi chini ya mstari wa umaskini. Mataifa yaliyoendelea lazima yafanye zaidi Baada ya kusikia simulizi hizo za kuvutia, Katibu Mkuu Guterres alitoa wito kwa mataifa yaliyoendelea kufanya zaidi, na kuyakumbusha juu ya jukumu lao la msingi katika kuwakaribisha wakimbizi na kuwapa nafasi ya kuanza upya katika mazingira salama, usalama mbali na hali duni wanazoweza kupata katika kambi au hali mbaya ya makazi. Aliongeza kuwa zamani alipokuwa akiongoza shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, kulikuwa na fursa maradufu za makazi mapya kwa wale wanaotoka katika kambi za wakimbizi na hali nyingine ngumu duniani kote. Kwa hivyo, alihimiza Mataifa zaidi kufungua mipaka yao kwa watu wanaotafuta hifadhi na kuwasaidia katika kutafuta hali bora ya maisha. Kati ya kesi zote za makazi mapya zilizowasilishwa na UNHCR kwa Mataifa mwaka 2021, asilimia 86 zilikuwa za waathirika wa mateso au unyanyasaji, watu wenye mahitaji ya kisheria na ya ulinzi wa kimwili, na kwa kiasi kikubwa wanawake na wasichana walio katika mazingira magumu. Zaidi ya nusu ya maombi yote yanahusu watoto. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, dunia ilifikia hatua ya kushangaza ya wakimbizi milioni 100 mwezi Mei, 2022, wiki 10 baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine kuwafukuza sio tu watu waliokimbia vita lakini pia ulisababisha ukosefu wa chakula duniani, pamoja na uhaba wa nafaka na mbolea.