Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tukio la mwanamfalme wa Saudia kudukua simu ya mkuu wa Amazon lichunguzwe- Wataalam

Uthibiti wa udukuzi unatengeneza taasisi imara za kifedha ambazo zinapelekea ustawi bora wa uchumi
UNODC
Uthibiti wa udukuzi unatengeneza taasisi imara za kifedha ambazo zinapelekea ustawi bora wa uchumi

Tukio la mwanamfalme wa Saudia kudukua simu ya mkuu wa Amazon lichunguzwe- Wataalam

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wameelezea wasiwasi wao mkubwa juu ya madai ya kwamba mwanamfalme wa Saudi Arabia alihusika katika udukuzi wa simu ya Jeffery Bezos ambaye ni mmiliki wa gazeti la Washington Post na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Amazon.

 

Wataalamu  hao huru, Agnes Callamard na David Kaye wamesema ya kwamba taarifa walizopokea zinadokeza “uwezekano wa kuhusika kwa mwanamfalme huyo katika kupeleka kiprogramu cha kiditali mwaka 2018 kuwezesha udukuzi wa simu hiyo ya Bezos kwa lengo la kushawishi au kunyamazisha gazeti hilo la Washington Post huko Saudi Arabia.”

“Tuhuma hizo zinaimarisha madai mengine ya mwenendo wa harakati za udukuzi dhidi ya watu wanaoshukiwa kuwa wapinzani na wale wenye umuhimu wa kimkakati kwa Saudi Arabia,” wamesema wataalamu hao kupitia taarifa yao iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi ikisema wanaofuatiliwa ni raia wa taifa hilo na wale wasio raia.

Miongoni mwa matukio mengine yaliyotajwa ni madai yanayoendelea kufuatiliwa ya kuhusika kwa mwanamfalme huyo wa Saudi Arabia kwenye mauaji ya mwandishi wa habari wa gazeti la Washington Post Jamal Khashoggi mwaka 2018.

"Shutuma za udukuzi wa simu ya Bwana Bezos na wengineo zinahitaji uchunguzi wa haraka sana na Marekani na mamlaka nyingine husika ikiwemo uchunguzi wa madai ya miaka kadhaa ya mwanamfalme huyo kulenga wapinzani,”  wamesema Bwana Kaye na Bi. Callamard.

Yaelezwa kuwa tarehe 1 mwezi Mei mwaka 2018 simu ya Bwana Bezos iliingiliwa kwa kutumia faili la video lililotumwa kwa njia ya WhatsApp kutoka kwenye akaunti binafsi ya mwanamfalme huyo wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman.

Kwa mujibu wa uchambuzi, Bwana Bezos na mwanamfalme huyo walibadilishana namba za simu mwezi mmoja kabla ya tukio daiwa hilo la udukuzi.