Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa IKEA wamaliza mvutano wa kuni baina ya wakimbizi na wenyeji Ethiopia

Mkaa unaotokana na miti unachangia katika uharibifu wa mazingira lakini sasa ukwajukwaju watumika huko Ethiopia kuandaa mkaa
FAO/Giulio Napolitano
Mkaa unaotokana na miti unachangia katika uharibifu wa mazingira lakini sasa ukwajukwaju watumika huko Ethiopia kuandaa mkaa

Mradi wa IKEA wamaliza mvutano wa kuni baina ya wakimbizi na wenyeji Ethiopia

Tabianchi na mazingira

Mradi wa ushirika unaosaidiwa na wakfu wa IKEA , wa kubadili magugu  ya mti wa Kiwajukwaju (Prosopis Juliflora )kuwa nishati ya kupikia na kujikimu kimaisha umekuwa mkombozi kwa wakimbizi na jamii zinazowahifadhi nchini Ethiopia. 

Katika eneo la Dollo Ado Ethiopia ambalo sehemu kubwa ni kame miti ya kikwajukwaju imesheheni ikichukuliwa kama magugu na wadudu hatari kutokana na aina yake ya kuvamia mahali na kusambaa lakini pia  wakati mwingine kuwadhuru wanyama wanaoila. Aden Abdullahi ni mkulima wa eneo hilo na anasema“miti hii inapokuwepo inatokomeza miti mingine yote,inakuwa peke yake na hilo ni tatizo kubwa. Mizizi yake inakwenda chini sana ardhini na inasambaa nakufanya kuwa vigumu kwa miti mingine kukua.”

Miti hiyo iliyoanza kupandwa Dollo Ado miaka 50 iliyopita inasambaa kwa haraka sana na kupokonya rasilimali zote kama nishati ya kuni katika eneo ambalo tayari lina ukame na kuleta changamoto kwa wakazi ambao ni wakimbizi 150,000 na jamii zinazowahifadhi. Moge Abdi Omar ni mratibu wa mradi  wa Wapydo ambao sasa ni suluhu ya mvutano huo, “tumeshuhudia  kumekuwepo na matatizo kati ya wakimbizi na jamii zinazowahifadhi migogoro mingi inatokea wanapokwenda msituni kusenya kuni na wakati huohuo kwenye maeneo ya makambi yote ya wakimbizi kama unavyoona yako matupu.”

Mradi huo unaosaidia na IKEA ni suluhu hasa kwa kugeuza magugu ya miti ya kikwajukwaju  kuwa mkaa na kuuza sokoni katika jimbo zima, na mradi una faida kubwa katika kulinda mazingira, kupunguza mizozo na kuinua uchumi wa jamii. 

Wanajamii wanaikata miti hiyo na kuiuza kwenye jumuiya ya ushirika wa wakimbizi ambao wanaitengeneza mkaa katika kituo maalum. 

Mkaa unaopatikana unatumika kwa muda mrefu kuliko mkaa wa kawaida kama anavyothibitisha mkimbizi kutoka Somalia Asha Ahmad ambaye anasema, “ukilinganisha na mkaa wa kawaida nimeona kwamba huu ni mzuri zaidi, lakini unahitaji kazi kubwa kuutengeneza. Nikianza kuupikia saa 8 mchana unawaka hadi saa moja usiku. Katika hayo masaa matatu naweza kupika chai na chakula cha jioni na hata saa moja baadaye mkaa bado unawaka naweza kupashia chakula.”

Wakimbizi wanasema hawakujua mengi mbali ya magugu kuhusu miti ya ukwajukwaju na  kutoivuna sababu ni hatari, lakini sasa wamen’gamua kwamba magugu hayo ni lulu kwao, maisha yao na jamii zinazowahifadhi.