Kampeni potofu mitandaoni kuhusu surua zimesababisha ongezeko la vifo- WHO

5 Disemba 2019

Vifo vinavyotokana na surua na maambukizi ya ugonjwa huo mwaka 2019 vinatarajiwa kuzidi vya mwaka uliopita wakati watu 142 wanaripotiwa kufariki dunia kutokana na ugonjwa huo unaozuilika, limesema shirika la afya ulimwenguni, WHO.

Kwenye onyo kuhusu viwango vya chini vya utoaji chanjo kwenye nchi kadhaa hali inayosababishwa na kampeni potovu kupitia mitandao ya kijamii, WHO ilisisitiza kuwa chochote kilicho chini ya asilimia 95 kinaleta hatari ya kutokea mlipuko.

Nchini Samoa ni asilimia 31 tu ya wakaazi wa kisiwa hicho walio na kinga dhidi ya surua  kwa mujibu wa WHO, ikiwa ni mfano wa athari za kampeni kwa njia ya mitandao ya kijamii ya kupinga chanjo dhidi ya surua

Hali hiyo imesababisha kuwepo kwa changamoto kubwa kiafya, huku hospitali na zahanati  zikiwa zimelemewa katika kuwahudumia wagonjwa hususan watoto walio chini ya miaka mitano na watu walio na magonjwa mengine ikiwemo kisukari.

Taarifa potofu zinazosambaa kwa njia ya mitandao ya kijamii zinaathiri maamuzi ya wazazi, iwapo wawapeleke watoto kupewa chanjo na matokeo yake ni kuwa watoto wanaambukizwa surua na wengine kufa, amesema mkurugenzi wa WHO anayehusika na masuala ya maradhi Dr Kate O’Brien

Kote duniani leo hii, chanjo dhidi ya surua ni karibu asilimia 86 imeongezeka kutoka asiliamia 72 mwaka 2000-hatua ambayo WHO inasema imesaidia kuokoa maisha ya watu milioni 23 katika kipindi hicho.

Licha ya kuwa ni mafanikio makubwa kwa afya ya umma na sababu ya kupungua kwa vifo vinavyotokana na surua tangu mwanzo wa karne kutoka 535,000 hadi 142,300 mwaka uliopita, hatua kidogo  zimepigwa katika kuboresha utoaji wa chanjo kwa karibu muongo mmoja kwa mujibu wa Dr O’ Brien.

Kutokana na takwimu za WHO za hivi punde zaidi visa vilivyoshukiwa na vile vilivyothibitishwa vya ugonjwa wa surua mwaka 2019 vilikuwa 614,915 vilivyoshukiwa na 413,308 vilivyothibitishwa, vikiwa vya juu zaidi kuliko vya mwaka 2018, ambavyo ni visa 483,215 na 333,445 mtawalia.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter