Serikali zisipochukua hatua dhidi ya mifumo ya fedha kutimiza SDGs itakuwa ndoto:UN/IMF/WTO

10 Aprili 2019

Mashirika zaidi ya sita ya kimataifa yakiongozwa na Umoja wa Mataifa likiwemo shirika la fedha duniani IMF, Benki ya Dunia na shirika la biashara duniani WTO kwa pamoja wametoa tahadhari katika ripoti yao mpya wakionya kwamba mifumo ya fedha ya kitaifa na kimataifa isipofanyiwa marekebisho na kufufuliwa basi itakuwa ndoto kwa serikali duniani kutimiza ahadi ya masuala muhimu kama kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kutokomeza njaa ifikapo 2030.

Katika ripoti yao “Ufadhili kwa ajili ya maendeleo endelevu 2019”  iliyotolewa leo mashirika hayo ya kimataifa yamesema pamoja na jitihada zinazotakiwa kufanyika kuna Habari njema: uwekezaji umeongezeka huku asilimia 75 ya wawekezaji binafsi wanaonyesha haja ya kufahamu uwekezaji wao umeathiri vipi dunia.

Hata hivyo kumekuwa na ongezeko la gesi ya viwandani ambayo imeongezeka kwa asilimia 1.3 mwaka 2017, uwekezaji katika nchi nyingi kuhusu hilo unashuka na nchi 30 zinazoendelea sasa ziko katika hatari ya kutumbukia kwenye mzigo wa madeni au zimeshatumbukia katika mzigo huo na wakati huohuo ukuaji wa uchumi kimataifa ukitarajiwa kufikia asilimia 3.

Ripoti hiyo imesisitiza kwamba “kubadili mfumo wa sasa wa ufadhili wa maendeleo endelevu sio tu kuhusu kuongeza uwekezaji, bali ufikiaji wa malengo ya kimataifa ya maendeleo unategemea mifumo ya fedha na mazingira bora ya kitaifa na kimataifa ya sera.”

Ripoti hiyo pia imeonya kwamba kuweka mazingira mazuri imekuwa changamoto, mabadiliko makubwa kwenye teknolojia, siasa na hali ya hewa vimebadili mfumo wa uchumi na jamii na taasisi za kitaifa na kimataifa ambazo zilisaidia kuwatoa mamilioni ya watu kwenye umasikini sasa zinahaha kwenda sanjari na mazingira. Na imani ya mfumo wa ushirikiano wa kimataifa hivi sasa inayumba moja ya sababu ikiwa ni kushindwa kwa mfumo huo kutimiza ahadi na kuwaacha watu wengi duniani wakiishi katika nchi ambazo pengo la kutokuwepo na usawa likizidi kupanuka.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter