Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa waipongeza Guinea-Bissau kwa kufanya uchaguzi wa amani.

Msichana akipiga kura mjini Bissau
Alexandre Soares.
Msichana akipiga kura mjini Bissau

Umoja wa Mataifa waipongeza Guinea-Bissau kwa kufanya uchaguzi wa amani.

Amani na Usalama

Naibu wa mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Guinea-Bissau, David McLachchlan-Karr ameipongeza Guinea-Bissau kwa uchaguzi uliofanyika leo jumapili kuwachagua wabunge.

Akizungumza na UN News, McLachlan-Karr ameuita uchaguzi huo “matokeo chanya kwa watu wa Guinea-Bissau. Watu wamejitokeza kupiga kura kwa idadi kubwa na wakapiga kura kwa amani. Hakukuwa na ripoti za matukio makubwa ya ukosefu wa usalama kote nchini”

Mstakabali

Kama ilivyoelezwa katika ripoti ya Katibu Mkuu iliyochapishwa mwezi Februari na makubaliano ya Baraza la Usalama yaliyopitishwa wiki iliyopita, Umoja wa Mataifa una matumaini uchaguzi huu utasaidia kumaliza mgogoro wa kisiasa ambao Guinea-Bissau imekabiliana nao tangu mwaka 2015.

Mwaka huo wa 2015, rais wa Guinea-Bissau, José Mário Vaz aliivunja serikali ya waziri mkuu Domingos Simões Pereira ambaye chama chake kilikuwa kimeshinda kwa viti vingi katika uchaguzi wa mwaka 2014. Tangu wakati huo kumeshakuwa na viongozi saba wa serikali.

Kwa mujibu wa McLachlan-Karr, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Baraza la usalama wamekuwa wakiufuatilia uchaguzi huo kwa ukaribu sana.

Matokeo ya awali yanategemewa kuanza kutangazwa jumatatu hii na matokeo rasimi yanategemewa jumatano. Chama ambacho kitashinda viti vingi zaidi ndicho kitaunda serikali.

Wapiga kura wakiwa katika mstari kwenda kuwachagua wabunge.
Alexandre Soares.

 

Uchaguzi

Katika mkutano wa waandishi wa habari karibu na mwisho wa siku ya uchaguzi, msemaji wa tume ya uchaguzi CNE amesema upigaji kura umefanyika kwa utulivu mkubwa na wapiga kura wamejitokeza kwa wingi japokuwa uhesabuji kura kwa ujumla haujakamilika.

Zaidi ya waangalizi wa kimataifa 130 wamesambazwa kote katika majimbo 8 ya nchi hiyo ya watu milioni 1.9. Kulikuwa na vyama 21 vilivyokuwa vinachuana, idadoi kubwa kuwahi kushiriki katika uchaguzi. Kwa sasa ni vyama vitano vilivyokuwa na uwakilishi bungeni.

Umoja wa Mataifa kusalia Guinea-Bissau hadi mwishoni mwa 2020.

Mwezi uliopita, baraza la usalama liliidhinisha maazimio yanayosema ofisi ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa ya kuleta amani nchini Guinea-Bissau, UNIOGBIS itatakiwa kufungwa mwishoni mwa mwaka 2020. Bwana McLachlan-Karr anasema Umoja wa Mataifa utautumia muda huo kuendelea kuhakikisha kunakuwa na utulivu na pia ujenzi wa amani.

 

TAGS: Guinea-Bissau, CNE, McLachlan-Karr