Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ulinzi wa raia DRC sio usalama tu, lishe na kipato pia:Mlinda amani Liuma

Mlinda amani, Ahmed Liuma (kulia kabisa) kutoka kikosi cha kujibu mashambulizi, FIB cha  ujumbe wa Umoja wa Mataifa huko DRC akielezea wakazi wa Mavivi, mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazini jinsi ya kulima mboga za majani kwa uendelevu kwa ajili ya kipato n
FIB/MONUSCO
Mlinda amani, Ahmed Liuma (kulia kabisa) kutoka kikosi cha kujibu mashambulizi, FIB cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa huko DRC akielezea wakazi wa Mavivi, mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazini jinsi ya kulima mboga za majani kwa uendelevu kwa ajili ya kipato na mlo wa kaya.

Ulinzi wa raia DRC sio usalama tu, lishe na kipato pia:Mlinda amani Liuma

Amani na Usalama

Mara nyingi tunaposikia ulinzi wa amani taswira inayokuja ni kubeba mtutu, kushika doria na hata kuwafurusha waasi, lakini kumbe ni zaidi ya hayo husuasn kwa jamii husika kwa mujibu wa mlinda amani wa Tanzania kutoka kikosi maalumu cha kujibu mashambulizi FIB cha  ujumbe wa  Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO. Flora Nducha anafafanua zaidi.

Mteule daraja la kwanza Ahmed Liuma, ni miongoni mwa walinda amani kutoka Tanzania walio kwenye kikosi cha FIB kilicho sehemu ya operesheni za Umoja wa Mataifa  katika eneo la Beni Mavivi jimboni Kivu Kaskazini.

Kazi wanazozifanya huko ni zaidi ya ulinzi wa raia kwani , wanaisaidia na kuielimisha jamii katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo kilimo cha mboga ambacho kinaleta ahueni sio tu katika lishe lakini pia kuisaidia kuinua kipato cha jamii.

Leo hii Liuma anatoa maelezo ya jinsi ya kupanda mbogamboga kwa wakazi wa eneo hilo la Mavivi akisema kuwa, “kama unataka kuongeza kipato, kufanya biashara, basi  utaongeza idadi ya mifuko, kutoka 10 utafikisha japo mifuko 50.  Na ukifikisha mifuko 50, ina maana 10 itakuwa ni ya kulisha familia na ile 40 itakayobakia, inayo uwezo wa kukupata kipato Faranga 10,000 kila siku.”

Akifafanua kwa wanawake hao wajasiriamali manufaa ya kiuchumi, Mteule daraja la kwanza Liume amesema, “mche mmoja kwa bei ya kawaida kabisa ya DR Congo kama unaamua kuuza, kwanza katika familia ya watu watano, unao uwezo wa kuvuna mashina matatu. Mashina matatu, ukivuna mboga zake zinatosha kulisha familia kwa siku moja. Lakini ukiwa na mifuko kama hii 9 au 10, leo ukivuna hapa mifuko mitatu ukala na familia, kesho hivyo hivyo, na kesho kutwa hivyo hivyo, ukirudi hapa mwanzo unakuta zile mboga zingine zimeshakomaa tayari kuvunwa. Ukiwa na mifuko yako 10 una uwezo wa kula kila siku mboga na hazitaisha.”

Mbali ya kilimo cha mboga walinda amani hawa wanasaidia pia katika mafunzo ya ushonaji, na hasa huduma za afya.