Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuzama kwa boti kwachochea wahamiaji kutaka kurejea nyumbani kwa hiari -IOM

Wahamiaji wakirudi nyumbani kwa msaada wa IOM
IOM
Wahamiaji wakirudi nyumbani kwa msaada wa IOM

Kuzama kwa boti kwachochea wahamiaji kutaka kurejea nyumbani kwa hiari -IOM

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM limesema kisa cha kuzama kwa meli mapema mwezi uliopita Djibouti mwezi uliopita na kusababisha vifo vya wahamiaji kutoka Pembe ya Afrika kimesababisha wahamiaji wengi kuliomba shirika hilo kuwarejesha nyumbani kwa salama

Meli hiyo ilizama mji wa Godoria uliopo katika jimbo Obock, kaskazini-mashariki mwa Djibouti ambapo watu 52 wakiwemo wanawake watatu walikufa maji. IOM inasema idadi kubwa ya waliokufa maji walikuwa wanatoka Ethiopia na manusura 16 wote nao kutoka Ethiopia walipatiwa huduma kwenye kituo cha shirika hilo mjini Obock kinachopata usaidizi pia kutoka Muungano wa Ulaya, EU.

Mratibu wa IOM nchini Djibouti Lalini Veerassamy amesema hadi sasa wameshasaidia wahamiaji 1327 kurejea nyumbani wakiwemo 16 ambao ni manusura wa chombo kilichozama mwezi uliopita.

Amesema idadi hiyo ni sawa na takribani theluthi moja ya wahamiaji 3,382 waliosaidiwa nchini Djibouti kurejea nyumbani kwa usalama mwaka jana wa 2018.

Veeressamy amesema bado kuna wahamiaji wengine wanaosubiri kurejea nyumbani akiwemo Bayan Mohamed Youssouf, kijana mwenye umri wa miaka 20 kutoka  Ethiopia.

Alipoulizwa sababu ya kuamua kurudi Ethiopia, Bayan amesema , “nililipa dola 450 kwa kwa msafirishaji haramu wa binadamu ili kuelekea Yemen. Nilikuwa ufukweni wakati wengine walipopanda boti iliyozama. Safari yangu ilivunjwa kwa sababu bahari ilichafuka. Sitaki kusafiri tena. Watu wengi walikufa. Nataka kurejea nyumbani.

IOM katika ripoti hii imebaini kuwa kijiografia Djibouti ni kivutio kikubwa kwa  vijana wa kiethiopia wanaotaka kuvuka Ghuba ya Aden kupitia Yemen, katika safari ya kuelekea Saudi Arabia.

Mpango wa pamoja wa muungano wa Ulaya na IOM EU-IOM umeweka mkakati wa kuwasaidia  wanaotaka kurejea nyumbani kwao katika kisimamia usawa, ulinzi na salama, wa uhamiaji kwa njia ya kuwezesha kurudi kwa hiari na utekelezaji wa sera na taratibu za uhamasishaji zinazoendelea