Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Surua yazidi kutesa Ulaya, WHO yasema “lazima tufikishe chanjo mashinani”

Muuguzi akitoa chanjo dhidi ya surua kwa mtoto nchini Paraguay
Picha:WHO/PAHO
Muuguzi akitoa chanjo dhidi ya surua kwa mtoto nchini Paraguay

Surua yazidi kutesa Ulaya, WHO yasema “lazima tufikishe chanjo mashinani”

Afya

Shirika la afya ulimwenguni, WHO, limesema idadi ya watu waliokumbwa na ugonjwa wa surua barani humo kwa mwaka 2018 ilikuwa ni kubwa zaidi katika muongo wa sasa.

Taarifa ya WHO kanda ya Ulaya iliyotolewa leo mjini Copenhagen, Denmark, imesema jumla ya watu 72 wakiwemo watu wazima na watoto walifariki dunia kutokana na surua barani Ulaya, kiwango ambacho ni mara 3 ya watu waliofariki dunia mwaka 2017.

WHO inasema kiwango hicho kimekuwa cha juu licha ya hatua zilizochukuliwa mwaka 2017 za kuongeza utoaji chanjo kwa watoto dhidi ya surua ambapo watoto walipatiwa dozi ya pili na kiwango cha utoaji chanjo hiyo kikafikia asilimia 90.

Shirika hilo linasema ingawa idadi kubwa zaidi ya watoto barani Ulaya wanapatiwa chanjo dhidi ya ugonjwa wa surua, kuliko wakati wowote ule, bado kasi ya utoaji wa chanjo hiyo inatofautiana kati ya nchi na ndani ya nchi .

Akizungumzia ripoti hiyo ya leo, Mkurugenzi wa WHO kanda ya Ulaya, Dkt. Zsuzsanna Jakab, amesema, “taswira ya mwaka 2018 inaonesha dhahiri kuwa kasi ya sasa ya kuongeza viwango vya utoaji chanjo haitoshelezi kukomesha kuenea kwa surua. Ingawa takwimu zinaonyesha ongezeko la utoaji chanjo katika ngazi ya kikanda, takwimu hizo hizo zinaonesha kuwepo kwa idadi kubwa ya wagonjwa na vifo kutokana na surua. Hii ina maana kuwa bado kuna pengo katika ngazi ya mashinani ambalo linakuwa ndio upenyo wa virusi vya ugonjwa huu.”

Dkt. Jakab amesema katu hawawezi kuwa na watu wenye afya duniani “kama ilivyoahidiwa kwenye dira ya WHO kwa miaka mitano ijayo iwapo hatufanyi kazi mashinani. Lazima tufanye kazi kwa ubora zaidi kulinda kila mtu dhidi ya ugonjwa huu ambao unaweza kuepukika kirahisi.”

WHO kanda ya Ulaya inachofanya sasa ni kushirikiana nan chi wanachama kwenye eneo hilo kusaidia kuimarisha mifumo ya utoaji chanjo mashinani hususan nchi za kipato cha kati.