Visa vya surua vyaongezeka ulimwenguni kwa sababu ya pengo la utoaji chanjo – Ripoti

29 Novemba 2018

Visa vya ugonjwa wa surua viliongezeka mwaka 2017, kutokana na milipuko isiyoisha ya ugonjwa huo katika maeneo kadhaa duniani, imesema ripoti iliochapishwa leo na shirika la afya ulimwenguni, WHO.

“Kwa sababu ya pengo la utoaji chanjo kitaifa au katika baadhi ya maeneo ndani ya nchi, surua iliripotiwa katika mabara yote na kusababisha vifo vya takribani watoto 110,000,” imesema ripoti hiyo.

WHO imesema visa vilivyoripotiwa vya surua viliongezeka kwa asilimia thelathini kutoka mwaka 2016. Amerika, kusini na eneo la Mediteranea na Ulaya yalikabiliwa na viwango vya juu kabisa huku eneo la kaskazini mwa Pacifiki ikiwa ni eneo pekee ambapo visa vya surua vilipungua.

“Kuongezeka kwa visa vya surua kunasikitisha, huku milipuko ya muda mrefu ikitokea katika maeneo na hususan katika nchi ambazo zilikuwa zimetokomeza surua au zimekaribia kutokomeza ugonjwa huo,” amesema Dkt. Soumya Swaminathan, Naibu Mkurugenzi wa miradi WHO.

Ameongeza kuwa bila juhudi za haraka za kuimarisha utoaji chanjo na kubaini jamii zilizo na viwango vya chini vya watoto waliochanjwa au hawajachanjwa, kuna uwezekano wa kupoteza maendeleo yaliokuwa yamepatikana ya kulinda watoto na jamii dhidi ya ugonjwa huo ambao unaweza kuzuiliwa.

Hapa ni Yemen, wagonjwa 20 wanatumia chumba kimoja hali ambayo inahatarisha kuambukizwa magonjwa kama vile surua na mengineyo yaambukizwayo kwa njia ya hewa. Kila mtu anastahili huduma bora ya afya.
OCHA/Eman
Hapa ni Yemen, wagonjwa 20 wanatumia chumba kimoja hali ambayo inahatarisha kuambukizwa magonjwa kama vile surua na mengineyo yaambukizwayo kwa njia ya hewa. Kila mtu anastahili huduma bora ya afya.

 

Surua ni ugonjwa hatari ambao unaambukiza, unaweza kusababisha madhara makubwa ya kiafya ikiwemo hali ya kuvimba kwa ubongo, kuhara na vichomi,  maambukizi ya masikio, na kusababisha kupoteza uwezo wa kuona. Watoto wachanga na watoto walio na utapiamlo na kinga ndogo wako hatarini kukumbwa na madhara ya kiafya na vifo.

Hata hivyo WHO inasema surua inaweza kuzuiwa kwa kupata dozi mbili salama na sahihi katika kuzuia surua.

WHO imetoa wito kwa nchi kuwekeza katika huduma ya utoaji chanjo ikilenga walio hatarini zaidi ambao ni jamii maskini na jamii zilizotengwa ikiwemo wanaokabiliwa na mizozo.

Aidha imetoa wito kuwepo kwa elimu ili kukabiliana na usambazaji wa habari potofu kuhusu chanjo.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter