Uingereza miongoni mwa mataifa manne Ulaya yaliyoshindwa kutokomeza Surua- Ripoti

29 Agosti 2019

Barani Ulaya ugonjwa wa Surua umesalia kuwa tatizo ambapo takwimu mpya zinaonesha kupungua kwa idadi ya mataifa yaliyokuwa yametokomeza ugonjwa huo.

Hili limekuwa hitimisho la kamisheni ya kanda ya Ulaya inayoshughulikia kutokomeza Surua na Rubella (RVC) kulingana na tathmini ya hali ya kila mwaka kwa mwaka 2018 iliyowasilishwa na nchi wanachama 53 wa ukanda wa Ulaya.

Kamisheni hiyo imeamua kuwa kwa mara ya kwanza tangu mchakato wa uhakiki uanze katika ukanda wa Ulaya mnamo mwaka 2012, nchi 4 yaani Albania, Jamhuri ya Czech, Ugiriki na Uingereza, wamepoteza hadhi yao ya kutokmeza surua.

Mwenyekiti wa Kamisheni hiyo, Dkt Günter Pfaff anataadharisha, “kurejea kwa maambukizi ya surua kunaleta wasiwasi.

Ikiwa usambazaji wa chanjo hautafikiwa katika eneo kubwa na kuendelezwa katika kila jamii, watoto na watu wazima wataathirika pasina umuhimu na wengine watafariki.

Hata hivyo wajumbe wamefurahi kuwa Austria na Uswisi wameifikia hadhi ya kutokomeza surua na wameonesha kukabiliana na maambukizi ya mlipuko angalau kwa miezi 36.

Kwa ukanda mzima jumla, kufikia mwaka 2018, nchi 35 zinafikiriwa kuwa zimefikia utokomezaji wa surua ikilinganishwa na nchi 37 kwa mwaka 2017. 

Ili kukabiliana na ugonjwa wa surua, msimamizi wa chanjo kwenye WHO Dkt. Katherine O’Brien, amesema

"Tuna chanjo salama na thabiti dhidi ya surua, Hutolewa kwa dozi mbili na kila mtoto kila mahali ambaye anaweza kupata chanjo anahitaji kupata chanjo hiyo. Hii ni chanjo ambayo inafanya kazi. Inamaanisha iwapo mtoto alipata chanjo uwezekano wa kuugua surua maishani ni mdogo. Kwa hiyo kila mzazi, kila familia, kila bibi au babu, kila jamii inahitaji kuunga mkono mfumo wa utoaji chanjo katika jamii yao na kila mtoto anahitaji kupelekwa.”

Nchi mbili zimekabili mlipuko wa ugonjwa kwa miezi 12 hadi 35, nchi 12 zimesalia na maambukizi ya surua na nchi 4 ambazo awali zilikuwa zimeutokomeza ugonjwa huo zimekabiliwa na ugonjwa huo kwa mara nyingine tena.

Kamisheni hiyo ya kukabili surua ba rubela Ukaya pia imehitimisha kuwa hali ya rubella imeimarika. 

Nchi 39 zimeweza kufikia hali ya kutokomeza ugonjwa huo ikilinganishwa na mwaka 2017.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud