EU yatoa dola milioni 6.7 kwa ajili ya shughuli za FAO Yemen.

Wakati vita ilipoanza nchini Yemen mwaka 2015, Yemen ilikuwa imeshawekwa katika kundi la nchi maskini zaidi duniani.
WFP/Reem Nada
Wakati vita ilipoanza nchini Yemen mwaka 2015, Yemen ilikuwa imeshawekwa katika kundi la nchi maskini zaidi duniani.

EU yatoa dola milioni 6.7 kwa ajili ya shughuli za FAO Yemen.

Ukuaji wa Kiuchumi

Wakati amani ya Yemen ikiwa katika hali mbaya na pia kukiwa na uhaba wa chakula, Muungano wa Ulaya na shirika la chakula na kilimo duniani FAO leo mjini Amman, Jordan, wametangaza mchango mpya uliotolewa na muungano wa ulaya wa kiasi cha dola  milioni 6.7 dola katika kuunga mkono kazi ya FAO ya kujenga uwezo wa Yemen kushughulikia masuala yanayosababisha uhaba wa chakula.

Fedha hizo zitasaidia Yemen kukusanya taarifa kuhusu njaa na utapiamlo na pia kufuatilia hali mbaya ya hewa au wadudu waharibifu pamoja na magonjwa, mambo ambayo yanachochea uhaba wa chakula.

Msaada huu pia utahusisha mafunzo kuhusu uhakika wa chakula, kipato na lishe, taarifa za masoko na mfumo wa taarifa za kijiografia. Hii itasaidia mapitio ya sera na mikakati ya sekta ya kilimo na uhakika wa chakula, uchambuzi wa taarifa za utafiti na kukusanya taarifa za mapema za tahadhari.

Taarifa iliyochapishwa katika ukurasa wa FAO imeeleza kuwa takwimu sahihi na taarifa kamili kuhusu vitisho dhidi ya maisha na uhakika wa chakula katika kaya ni muhimu kuweza kufahamu ni wapi na wakati gani msaada wa kibinadamu unahitajika zaidi.

Salah El Hajj Hassan mwakilishi wa FAO nchini Yemen amesema pamoja na kwamba inaonekana majanga ya sasa yataendelea kuitishia Yemeni lakini, “uwepo wa taarifa za uhakika na za muda muafaka si tu zinamaanisha tunaweza kuchukua hatua vizuri wakati janga linapoathiri uhakika wa chakula kama ilivyo sasa bali pia ni msingi ambao kwao serikali, mashirika ya misaada ya kibinadamu na maendeleo wanaweza kukuza usitahimilivu wa watu ili kukabili uhaba wa chakula katika siku za usoni”

Balozi wa Mungano wa Ulaya nchini Yemen Antonia Calvo Puerta amesema,” Ukubwa tatizo la uhaba wa chakula Yemen unaweka ugumu mkubwa kwa watu wengi ambao wako katik uhitaji mkubwa wa misaada ya kibinadamu. Kwa msingi huo muungano wa Ulaya una uhakika kuwa ushirikiano huu mpya na FAO utafaidisha watu wa Yemeni kwa kiasi kikubwa.”