Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vyombo vya uvuvi vyakaguliwa kulinda samaki

Uvuvi wa samaki nchini Korea. Picha ya UN/M Guthrie

Vyombo vya uvuvi vyakaguliwa kulinda samaki

Tabianchi na mazingira

Hii leo ni siku ya kimataifa ya kukabiliana na uvuvi haramu na usiodhibitiwa ambao unatishia uwepo wa samaki na viumbe vingine vya bahari vilivyo hatarini  kutoweka.

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO linasema ingawa uvuvi huo haramu wakadiriwa kuwa na thamani ya dola bilioni 23 kila mwaka, bado gharama yake kwa maisha ya binadamu na mazingira ni kubwa kupindukia.

FAO inasema uvuvi huo husababisha pia utumikishaji wa watu, utumwa, usafirishaji wa madawa ya kulevya na ukwepaji wa kodi.

Eneo ambalo uvuvi huo ulikithiri miaka ya 1960 ni katika bahari nyeusi iliyo kati ya Ulaya Mashariki na bara la Asia, na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na kutoweka kwa samaki miaka ya 1980.

Hata hivyo hivi sasa FAO  inasema Bulgaria, Romania na mataifa mengine ya Muungano wa Ulaya yamechukua hatua kudhibiti uvuvi haramu, usiodhibitiwa na usioripotiwa, IUU.

 Dimitar Petkov, ni mtaalamu mkuu wa mamlaka ya uvuvi nchini Bulgaria.

 “Hivi sasa kuna ukaguzi unafanyika ili kuthibitisha nyaraka za chombo cha uvuvi, vyeti vya uvuvi wa kibiashara pamoja na vifaa vya uvuvi wa samaki. Halikadhalika tunakagua nyaraka ya mwenendo wa uvuvi, kile ambacho kimejazwa na iwapo kila kitu kinaendana na masharti ya sheria za uvuvi na ukuzaji wa mazao ya baharini.”

Shirika hilo limesema ingawa kukabiliana na uvuvi huo ni changamoto kubwa, bado kuna maridhiano yamefikiwa katika siku za karibuni ili kushirikiana na kuondokana na tatizo hilo.

Maadhimisho ya siku hii yatafuatiwa na mkutano huko Sofia, Bulgaria hapo kesho tarehe 6 kwa lengo la kutoa fursa mpya ya kukubaliana kanuni, kutekeleza mikakati iliyopitiwa na pia kuimarisha ushirikiano wa kutokomeza uvuvi haramu huko bahari nyeusi.