Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa FAO waleta nuru kwa wakulima huko Ibb nchini Yemen 

Mkulima Rashed kutoka jimbo la Ibb nchini Yemen akikumbuka enzi za utoto wake akishiriki kilimo na baba yake.
UNIFEED/FAO/Video Capture
Mkulima Rashed kutoka jimbo la Ibb nchini Yemen akikumbuka enzi za utoto wake akishiriki kilimo na baba yake.

Mradi wa FAO waleta nuru kwa wakulima huko Ibb nchini Yemen 

Tabianchi na mazingira

Nchini Yemen katika jimbo la kusini-magharibi, la Ibb, mbinu mpya za umwagiliaji kwa kutumia mradi wa kusukuma maji kwa nguvu za sola umeleta nuru mpya na matumaini kwa wakazi wa eneo hilo.

Kutana na mkulima Rashed kutoka jimbo la Ibb nchini Yemen akikumbuka enzi za utoto wake akishiriki kilimo na baba yake, hata hivyo vita nchini Yemen vimesababisha uhaba wa maji na nishati ya mafuta waliyokuwa wanatumia kuendesha pampu za umwagiliaji shambani. 

Asilimia 70 ya wananchi wa Yemen ni wanaishi vijijni na kilimo ndio tegemeo lao la kupata kipato. 

Rashed anasema “tumekuwa tukimwagilia mashamba yetu kwa kutumia maji ya mvua ya msimu na pia kutoka mtoni, lakini sasa hakuna tena na mazao yetu yanakauka.” 

Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Muungano wa Ulaya (EU) wamesikia kilio chao na kuanzisha mradi wa pampu za umwagiliaji kwa kutumia nishati ya sola ambao unasambazaji maji kwa kaya 400. 

Kila wiki ya pili, bomba linaloelekeza maji shambani mwa Rashed hufunguliwa na kumwagilia shamba hilo ambapo mkuu wa chama cha watumiaji maji, (WUA), Murtada Ahmed anasema,  “wakulima wengi kama Rashed walikuwa wameathirika sana kabla msaada wa FAO. Kusukuma maji bila kutumia nishati ya mafuta kumebadili mno maisha yetu.” 

Joel Munywoki, ni mshauri mkuu wa kiufundi FAO na anasema, “Wakulima wengi wametupatia taarifa nzuri kuwa pampu ya sola ndio jambo halisi. Hawahitaji tena kununua nishati ya mafuta, kwa kuwa pampu ipo na kuna jua. Yemen inapata jua mwaka mzima. Kwa hiyo wana pampu, na wanapata maji ambayo yanakwenda moja kwa moja shambani. “ 

Na kwa Rashed yeye ni shukrani kwa kuwa sasa ameweza kulima mazao mengi ya chakula na mengine anauza sokoni ili kujipatia kipato na zaidi ya yote, Anasema “Watoto wangu wanasoma shuleni. Naona mustakabali bora kwao. Asante Mungu, maisha yetu yamebadilika baada ya kufungwa kwa mfumo wa pampu za maji zinazotumia nishati ya sola. Hatuna tena hofu ya kununua mafuta kwa ajili ya umwagiliaji.”