Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchini Kenya, kinyesi cha binadamu chatumika kutengeneza mkaa mbadala

Mkaa unaotokana na miti unachangia katika uharibifu wa mazingira lakini sasa ukwajukwaju watumika huko Ethiopia kuandaa mkaa
FAO/Giulio Napolitano
Mkaa unaotokana na miti unachangia katika uharibifu wa mazingira lakini sasa ukwajukwaju watumika huko Ethiopia kuandaa mkaa

Nchini Kenya, kinyesi cha binadamu chatumika kutengeneza mkaa mbadala

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP linasema mkaa unaotengenezwa kwa kutumia kinyesi cha binadamu unadumu mara mbili zaidi ya mkaa wa kawaida na zaidi ya yote kiwango chake cha uchafuzi wa mazingira ni kidogo mno ikilinganishwa na kiwango cha uchafuzi wa hewa cha mkaa unaotokana na miti. 

Mkaa huo unatengenezwa na kampuni  iitwayo Sanivation, inatengeneza mkaa mbadala kwa kutumia kinyesi cha binadamu na hivyo kutunza misitu na usafi kwa wakati mmoja.

Mwanzilishi mwenza wa kampuni hiyo, Emily Woods akihojiwa na shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP, anasema watu wengi duniani baada ya kujisaidia hawafikirii hatma ya kinyesi.

Ametolea mfano  nchini Kenya ambako asilimia 95 ya kinyesi cha binadamu kinatekelezwa badala ya kuwekewa dawa za kuua vijidudu kabla hakijaachiwa katika mazingira.

Lakini ni vipi Sanivation wanatumia kinyesi kutengeneza mkaa? Bi. Woods anasema.“Tunachukua kinyesi cha binadamu na kukiweka kwenye joto kali kwa kutumia nishati ya joto itokanayo na paneli za sola zilizounganishwa na kuwa kama ungo mkubwa. Joto linatosha kuua vijidudu. Kwa hivyo katika mchakato huo si tu unaua vijidudu bali unakibadilisha kinyesi kuwa kigumu.

Bi. Woods anasema hatua hiyo inafuatiwa na kuchanganya kinyesi kigumu na vitu vingine kama unga wa mkaa, mabaki ya mbao na takataka nyingine za namna hiyo kisha wanazikandamiza na kutengeneza aina mpya ya mkaa“Hauonekani kama kinyesi, haunuki wala kuungua kama kinyesi. Unaonekana kama mkaa tu. Kwa hivyo ni mbadala mjarabu.”

Na anahitimisha kwa kusisitiza kuwa matumizi ya mkaa mbadala kama huu, yanasaidia kuokoa miti na pia kuwahakikishia watu usafi kwani mkaa ukiuzwa wanapata fedha za kuendelea kusafisha mazingira.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.