Kinyesi si taka tena Kakuma bali ni faida.

28 Machi 2019

Wakimbizi Kakuma nchini Kenya wameshukuru na kupongeza mradi wa nishati mbadala unaoendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR Kenya, mfuko wa Bill Gates na shirika la Sanivation. 

Mradi huo unaotumia kinyesi cha binadamu kutengeneza nishati mbadala umebadilisha maisha ya wakimbizi hao.

Video ya Shirika la UNHCR inamwonesha Lucy Ivere akiandaa mlo. Moto katika jiko lake la udongo umekolea kweli kweli na katika chungu, mboga ni samaki. Mlo wa Lucy unaiva haraka na unatumia gharama ndogo. Anatumia nishati iliyotengenezwa kwa mchanganyiko wa kinyesi cha binadamu na vumbi la mkaa.

(Sauti ya Lucy Ivere)

“Mkaa huu una utofauti na huo mkaa mwingine, kwasababu huu mkaa unawaka sana, na ina moto mwingi watoto hawawezi kuchelewa kula. Unaweza kumaliza kupika chakula chako chote na ukamaliza kazi na huo moto ukawa unawaka bado.”

Imani Daudi, mkimbizi kutoka DRC ni miongoni mwa wanaokusanya kinyesi hicho kinachotumika kutengeneza nishati mbadala ya mkaa wa kawaida.

(Sauti ya Imani Daudi)

“Kazi hii tunaingia asubuhi tunakusanya kinyesi hapa katika jamii, tunafanya kazi siku tano kwa wiki.”

Kinyesi kinawekewa dawa, kinachanganywa na vumbi la mkaa kisha kinakandamizwa ili kutengeneza vitufe vya mkaa kwa ajili ya matumizi. Ni suluhisho la nishati lisilo na gharama kubwa na pia linahifadhi mazingira.

Syrus Mutua mtaalamu wa mkaa huo anasema kutoka shirika la Sanivation,

(Sauti ya Syrus Mutua)

“Moja ya faida ya aina hii ya mkaa ni kuwa unawaka mara mbili ya mkaa wa kawaida, unachafua hewa kidogo mno kulinganisha na mkaa wa kawaida, muhimu zaidi kimazingira tunaweza kuokoa miti 88 kwa kila tani moja ya mkaa wetu tunaotengeneza.”

Kwa mujibu wa UNHCR mradi huu siyo tu unahifadhi mazingira, kutoa nishati mbadala bali pia umewapa vijana ajira na kuwainua kiuchumi.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud