Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Je wajua kuwa senti 20 ya dola kwa kila mtu itaokoa mamilioni ya watoto wachanga ifikapo 2030?

Mtoto mchanga wa umri wa siku mbili akiwa amelala pembezoni mwa mama yake katika wodi ya wazazi huko Rajasthan India.
UNICEF/Prashanth Vishwanathan
Mtoto mchanga wa umri wa siku mbili akiwa amelala pembezoni mwa mama yake katika wodi ya wazazi huko Rajasthan India.

Je wajua kuwa senti 20 ya dola kwa kila mtu itaokoa mamilioni ya watoto wachanga ifikapo 2030?

Afya

Takribani watoto milioni 30 huzaliwa wakiwa pengine njiti au wadogo kupindukia au hata wanaugua kila mwaka na hivyo kuwa kuhitaji huduma maalum ili waweze kuishi, limesema shirika la afya duniani, WHO katika ripoti mpya iliyozinduliwa leo huko New Delhi India.

“Pindi linapokuja suala la watoto na mama zao, huduma sahihi wakati sahihi na mahali sasa zinaweza kuleta tofauti kubwa,” amesema Omar Abdi, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF ambao ndio wametoa ripoti hiyo iliyopatiwa jina Ripoti hiyo imepatiwa jina Ishi na Chanua: Kubadilisha huduma kwa watoto wazaliwao wadogo na wagonjwa.

Hata hivyo amesema “bado  mamilioni  ya watoto wachanga wagonjwa na wanawake wanakufa kila mwaka kwasababu tu hawapati huduma bora ambayo ni haki yao na ambayo pia ni wajibu wetu wa pamoja kuwapatia.”

Kwa muhtasari ripoti imebaini kuwa miongoni mwa watoto wachanga wanaozaliwa wakiwa  hatarini ya kufariki dunia au kupata ulemavu, ni wale ambao wanazaliwa njiti, wanapata tatizo la ubongo wakati wanazaliwa au kupata maambukizi ya bakteria na zaidi ya yote gharama za kifedha na kisaiokolojia ambazo zinakumba familia zao zinaweza kuwa na madhara makubwa katika makuzi yao na uwezo wao wa kuzungumza.

Ripoti inasema kuwa bila huduma maalum idadi kubwa ya watoto wachanga wanaozaliwa na matatizo hayo hawatamaliza mwaka wa kwanza wa uhai wao ikisema mwaka 2017, “watoto wachanga milioni 2.5 walikufa, wengi wao kutokana na magonjwa yanayozuilika, takribani theluthi mbili ya idadi hiyo walizaliwa njiti.”

Mtoto mchanga akipokea chanjo ya polio katika hospitali mjini Abidjan, Ivory Coast.
UNICEF/Olivier Asselin
Mtoto mchanga akipokea chanjo ya polio katika hospitali mjini Abidjan, Ivory Coast.

 

Hata hivyo ripoti imesema huduma bora ya malezi kwa watoto wenye matatizo hayo itasaidia waishi bila matatizo ambapo inaelezwa hilo likifanyika, ikifika mwaka 2030, maisha ya wanawake, watoto wachanga na njiti milioni 2.9 yanaweza kuokolewa katika mataifa 81.

“Kinachotakiwa ni mikakati bora. Mathalani iwapo wahudumu wa afya wanaohudumia watoto ndio hao hao wanahudumia mama zao kuanzia wakati wa uchungu, kuzaliwa na baada ya hapo, ni rahisi kubaini tatizo mapema,” imesema ripoti hiyo.

Mapendekezo mengine ni huduma ya saa 24 siku saba kwa wiki kwa watoto wachanga, mafunzo kwa wauguzi ili washirikiane na familia wakati wa utoaji huduma pamoja na kutenga fedha za kutosha ikitakiwa nyongeza ya dola senti 20 kwa kila mtu ikielezwa kuwa inaweza kuokoa watoto wachanga kati ya wawili hadi watatu katika nchi zinazoendelea ifikapo mwaka 2030.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.