Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya kutokuwa na usawa inatishia amani, usawa na maendeleo: Wataalam UN

Kamati ikitayarisha muswada wa kimataifa kuhusu haki
UN Photo.
Kamati ikitayarisha muswada wa kimataifa kuhusu haki

Hali ya kutokuwa na usawa inatishia amani, usawa na maendeleo: Wataalam UN

Haki za binadamu

Wataalam Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu wametoa wito wa kuimarisha haraka juhudi za kukabiliana na tofauti za kiuchumi na ubaguzi.
 

 

Wito huo wameutoa leo kupitia taarifa iliyotolewa mjini Geneva Uswisi kama sehemu ya kuadhimisha  miaka 32 ya tamko la haki kuhusu maendeleo inayoadhimishwa kila Disemba 4 ambapo wamesisitiza umuhimu wa kuendeleza jamii ambazo hazina usawa na kuimarsiha usawa wa fursa na matoke ya ndani na baina ya nchi.

Taarifa imesema kuwa kutokuwa na usawa pamoja na ubaguzi ni baadhi ya changamoto zinazokabili dunia wakati huu, na sio tu ni kizuizi cha kupata haki  ya maendeleo lakini pia inasalia kama tisho kubwa kwa amani, usalama, na haki za binadamu duniani. Na ndio  kichocheo kikubwa cha uhamiaji.
 
Miaka zaidi ya 30 iliyopita, tamko la haki ya maendeleo lilibaini  kuwa kutokuwa na usawa ni kikwazo katika kufikia haki za binadamu. 

Tamko hilo ndio maana limeanisha umuhimu wa kuhakikisha usawa katika usambazaji wa maendeleo na usawa katika fursa za kupata huduma muhimu katika maisha ikiwemo, elimu, huduma za kiafya, chakula, pamoja na makazi.
 
Wataalam wamegusia kuwa leo "tunaishi katika dunia yenye mali zaidi lakini hakuna usawa zaidi ya awali. Haki za kijamii na kiuchumi zinabinywa kwa watu wengi kote ulimwenguni ikiwemo watu takriban milioni 800 ambao wanaishi katika umaskini uliokithiri."

Wataalam hao wamesema, baadhi ya ripoti zilizochapishwa zinaonesha kuwa asilimia 82 ya mali zilizobuniwa 2017 ziliishia kwa asilimia 1 ya watu kwenye dunia wakati asilimia 50 wa chini hawakuona ongezeko lolote.
 
Pia wamesema kuna tofauti kati ya uwezeshwaji kiuchumi wanaume na wanawake ambapo wanawake hukumbana na ubaguzi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kijamii, kitamaduni pamoja na kisiasa.
 
 Kwa mantiki hiyo wamesema mataifa ni lazima yaheshimu wajibu wao na kukabilian na aina zote za ubaguzi na ukosefu wa usawa ili kuhakikisha mustakabali ambao unazingatia maendeleo jumuishi na sawa.