Mantiki ya ibara ya 24 ni kutoa mwanya kwa watu kuwa na uhuru binafsi na kupata mwanya wa kupumzika na familia zao

5 Disemba 2018

Kama kawaida tunaendelea kuchambua ibara baada ya ibara za tamko la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa.

Ibara ya 24 ya tamko la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa linalotimiza miaka 70 mwezi huu, inasema kila mtu ana haki ya kupata mapumziko na burudani ikiwemo kuwa na muda wenye ukomo wa kufanya kazi na pia kupatiwa likizo yenye malipo. Katika nchi mbalimbali zilizoridhia tamko hilo la haki za binadamu, sheria zinazoendana na ibara hii zipo lakini changamoto kubwa ni utekelezaji wake. Mwanasheria Tito Magoti wa kituo cha sheria na haki za binadamu LHRC Tanzania akizungumza na Arnold Kayanda anasema mantiki ya ibara hii ya 24 ni kutoa mwanya kwa watu kuwa na uhuru binafsi na kupata mwanya wa kupumzika na familia zao. Pia anasema kuwa tafiti zinaonesha uwepo wa malalamiko kwa wafanyakazi hasa walioko katika sekta binafsi kwamba hawapati mapumziko na hata wanaopata likizo hawalipwi inavyostahili.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter