Skip to main content

Mamia ya wahamiaji walio katika msafara wasaidiwa na IOM kurejea Amerika ya Kati

Msafara wa wahamiaji wa Amerika ya kati ukipita Chiapas Mexico (2018)
IOM / Rafael Rodríguez
Msafara wa wahamiaji wa Amerika ya kati ukipita Chiapas Mexico (2018)

Mamia ya wahamiaji walio katika msafara wasaidiwa na IOM kurejea Amerika ya Kati

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji, IOM limekuwa likiwasaidia mamia ya wahamiaji walioko katika msafara kutoka mataifa ya Amerika kurejea nyumbani kwa hiyari, mpangilio na usalama.

Tangu Novemba 4 mwaka huu IOM imeshafanikiwa kuwarejesha mamia ya wahamiaji kutoka Amerika ya Kati ambao walikuwa sehemu ya msafara wa wahamiaji wanaokwenda Amerika kupitia Mexico.

Hadi kufikia jana kwa mujibu wa IOM wahamiaji 453 asilimia 84 wakiwa ni wanaume waliokuwa kwenye msafara huo waliomba na kupata msaada wa IOM kurejea katika nchi zao za Honduras, El Salvador na Guatemala na watoto 25 wahamiaji wasiokuwa na mzazi au mlezi yoyote walilereshwa kwa ndege.

Ukusanyaji wa taarifa zao na uandikishaji wa wahamiaji hao unafanyika kwenye mji wa Tecún Umán Guatemala, Tapachula, Mexico City, na mjini Tijuana México.

Zaidi ya wahamiaji 300 kutoka Amerika ya Kati wameelezea nia yao ya kutaka kurejea Tijuana,na IOM inaratibu njia bora na yenye hadi ya wahamiaji hao kurejea nyumbani.

Na kwa wahamiaji hao ambao wanataka kurejea nyumbani wanapatiwa ushauri nasaha ,kupimwa na kuhojiwa na IOM, ili kubaini hali yao kabla ya kufanya maamuzi ya kuwarejesha nyumbani.

Mpango huu ambao unafadhiliwa na idara ya Marekani ya idadi ya watu, wakimbizi na wahamiaji (PRM) unaratibiwa na IOM kwa kushirikiana na nchi zote watokako wahamiaji hao.

Na wakati wa safari yao ya kurejea nyumbani wahamiaji hao hupewa chakula na ushauri nasaha, na pindi wanapovuka mpaka wanapowasili katika kituo maalumu cha mapokezi nchini El Salvador, Honduras na Guatemala, wahamiaji hao hupewa vifaa vya usafi na kujisafi, na mara nyingi fedha za usafiri wa kuwafikisha nyumbani.

Wengi wa wahamiaji waliohojiwa wamesema walifahamu kuhusu maandalii ya msafara huo yanayofanyika kupitia mitandao ya kijamii na televisheni, na wengi waliamua kujiunga katika makundi ya ndugu na majirani na kuingia katika msafara huo.