Maji safi Malaysia yapaswa kuwa haki ya kila mtu:UN

27 Novemba 2018

Mtaalam wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu ameitaka serikali ya Malaysia kutomuacha nyuma mtu yeyote yule na pia kufanya juhudi za kupunguza pengo la kutokuwa na usawa katika kupata huduma za maji na kujisafi.

Katika taarifa iliyotolewa leo mjini Kuala Lumpur, mji mkuu wa Malaysia, baada ya ziara ya kikazi nchini humo, mtaalam huyo maalum kuhusu haki za maji safi ya kunywa na kujisafi Bw. Leo Heller amesema ingawa Malaysia imepiga hatua katika nyanja ya maji na kujisafi  ambapo takwimu zinaonyesha kuwa huduma hiyo inakaribia kupatikana katika sehemu za miji, lakini inafaa sasa kumulika kwa wengine ambao hawajapata huduma hiyo akisisitiza kuwa raia wote wa nchi hiyo wana haki ya kupata huduma hizo sawa.

Ameongeza kuwa baadhi ya watu hawakupata huduma hizo kwa sababu hawajiwezi kiuchumi ama huishi katika makazi duni au maeneo ya vijijini ama hata kuwa na mielekeo tofauti na wengine.

Amebaini kuwa kujumuisha makundi yote  ya jamii kupitia haki za binadamu ndiyo ufunguo wa kutoa mchango sawa wa maji na huduma za kujisafi bila ubaguzi. Akisema hii ni  katika mwelekeo wa kutomuacha mtu yeyote nyuma jambo ambalo ni muhimu katika kufanikisha ajenda ya maendeleo endelevu au SDG’s na kutekeleza mpango wa nchi hiyo wa miaka 11 wa maendeleo.

Hatua muhimu ya kufanikisha hilo ni kumuhusisha kila mtu ili kuweza kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu bila kuwabagua watu ambao wanapuuzwa au wanatengwa.

Mtaalam huyo pia ameelezea wasiwasi wake kuhusu tukio la hivi majuzi ambapo serikali ilitangaza kuwa  haitaridhia  mkataba wa kimataifa wa kuondoa aina zote ya ubaguzi wa rangi ICERD nchini humo akisema kuwa ni hatua ya kusikitisha ambayo inakwenda kinyume na azma ya serikali.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter