Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kufukuzwa Malaysia kwa wasaka hifadhi kutoka Mynamar, kwatia hofu UNHCR

Mtoto wa kike akiwa nje ya makazi yao kwenye kambi ya wakimbiz iwa ndani huko Myanmar
© UNICEF/Minzayar Oo
Mtoto wa kike akiwa nje ya makazi yao kwenye kambi ya wakimbiz iwa ndani huko Myanmar

Kufukuzwa Malaysia kwa wasaka hifadhi kutoka Mynamar, kwatia hofu UNHCR

Haki za binadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema lina wasiwasi mkubwa juu ya vitendo vya raia wa Myanmar wanaosaka hifadhi nchini Malaysia kufukuzwa na na kurejeshwa makwao jambo linalotia hatarini usalama wao.

Msemaji wa UNHCR mjini Geneva, Uswisi Shabia Mantoo ametoa kauli hiyo leo akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema shirika lake linapokea ripoti za kutisha za mashinikizo kwa raia wa Myanmar nchini Malaysia kuwa tangu mwezi Aprili mwaka huu wanatakiwa kurudi nyumbani hata wale wanaosaka hifadhi ya kimataifa.

Raia wanalazimishwa kurejea kusiko na amani

“Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita pekee, mamia ya raia wa Myanmar wameripotiwa kurudishwa nyumbani na mamlaka za Malaysia kinyume na utashi wao,” amesema Bi. Mantoo akiongeza kuwa aina hiyo ya kurejeshwa nyumbani kwa wakimbizi na wasaka hifadhi ni saw ana kufukuzwa.

Kwa mujibu wa UNHCR, tukio la hivi karibuni zaidi la kurejeshwa nyumbani kinguvu kimetokea mwishoni mwa wiki hii. “Kwa mujibu wa taarifa zilizopokewa na UNHCR, msaka hifadhi mmoja kutoka Myanmar alirudishwa nyumbani kinguvu tarehe 21 mwezi huu wa Oktoba licha ya UNHCR kuzuia kitendo hicho.”

Bi. Mantoo amesema UNHCR inaendelea kutoa wito kwa Malayasia kusitisha mara moja urejeshaji nyumbani kinguvu kwa raia wa Myanmar wanaosaka usalama.

“Kuwarejesha nyumbani Myanmar ni sawa na kuwatia hatarini. Watu wanaokimbia Myanmar lazima wapatiwe fursa ya kuingia nchi nyingine na kupata hifadhi na walindwe ili wasifukuzwe,” amesema afisa huyo wa UNHCR.

Ametamatisha akisema, raia wa Myanmar ambao tayari wanaishi ughaibuni hawapaswi kulazimishwa kurejea nyumbani pindi wanaposaka hifadhi ya kimataifa na kwamba Kanuni ya kutofukuza ni nguzo ya sheria ya kimataifa na inabana nchi zote.

Hali ya Myanmar si salama

UNHCR inasema hali nchini Myanmar ndio chanzo cha watu kulazimika kukimbia kusaka usalama kwenye maeneo mengine ya nchi hiyo au hata kuvuka mipaka.

Shirika hilo limetoa wito kwa mamlaka za Malaysia kuzingatia wajibu wake kwa sheria za kimataifa  na kuhakikiha zinaheshimu haki za watu wote wanaohitaji hifadhi ya kimataifa.

“Tunasisitiza wito wetu kwa nchi kwenye ukanda huo wa Asia kuendelea kupatia hifadhi raia wa Myanmar wanaokimbilia maeneo salama. Hii pia inajumuisha kuondokana na tabia ya kuwasweka watu rumande wasaka hifadhi na wakimbizi kutoka Myanmar,” amesema Bi. Mantoo.