12 Oktoba 2018
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha uamuzi wa serikali ya Malaysia wa kufuta adhabu ya hukumu ya kifo nchini humo.
Katika ujumbe wake kwa serikali ya Malaysia, Katibu Mkuu Guterres, amesema kuwa uamuzi huo wa baraza la mawaziri wa Malaysia, umechukuliwa wakati muafaka ambapo dunia imeadhimisha siku ya kimataifa ya kupinga hukumu ya kifo tarehe 10 Oktoba.
Bw Guterres, amesema kuwa uamuzi huu ni hatua moja mbele katika mchakato mzima wa dunia wa kufuta hukumu ya kifo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa mataifa yote ambayo bado yana hukumu ya kifo katika vitabu vyao vya sheria kufuata mfano wa Malaysia.