‘Rejea nyumbani salama,’ yamulika ukatili dhidi ya wanawake kwenye usafiri wa umma Sri Lanka

Katika hali ya usafiri kama hii, wanawake wanakuwa hatarini zaidi kukumbwa na ukatili wa kingono
ESCAP /Bhar Sudip
Katika hali ya usafiri kama hii, wanawake wanakuwa hatarini zaidi kukumbwa na ukatili wa kingono

‘Rejea nyumbani salama,’ yamulika ukatili dhidi ya wanawake kwenye usafiri wa umma Sri Lanka

Wanawake

Nchini Sri Lanka, shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu, UNFPA na shirika moja liitwalo Cheer Up Luv wanafanya kampeni ya pamoja kukabiliana na unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanawake kwenye usafiri wa umma.

Hatua hiyo inatekelezwa ikiwa ni sehemu ya kampeni inayoendelea duniani ya siku 16 ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia kwa kuzingatia kuwa nchini Sri Lanka asilimia 90 ya wanawake wamekumbana na ukatili wa kingono kwenye usafiri wa umma, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na UNFPA.

Kupitia ushirika huo, UNFPA na Cheer Up Luv kila siku wanachapisha habari moja kupitia mitandao ya kijamii inayoonyesha madhila hayo.

“Habari hiyo inakuwa kwa mfumo wa filamu, picha na inaelezea simulizi ya ukatili wa kingono kutoka kwa wanawake wenyewe, ukatili wanaokabilana nao kwenye mabasi ya umma au treni wakati wakisafiri,” imesema taarifa iliyotolewa na UNFPA jijini New York, Marekani.

Miongoni mwa filamu  hizo ni ile iliyopatiwa jina, ‘Rejea nyumbani salama’ ambayo ni mjumuisho wa simulizi za wanawake 16 za kile walichokabiliana nacho.

Mathalani msichana  mmoja anasimulia ukatili  uliompata akiwa na umri wa miaka 12,  akisema"ninachotaka kusimulia kilinipata nikiwa na umri wa miaka 12. Siku moja nikisafiri kwa basi mwanaume mmoja alikuwa ameketi nyuma yangu. Nilikuwa nimevaa sare za shule, narejea  nyumbani nikiwa na mdogo wangu wa kiume. Alijaribu kufungua zipu  yake, akijaribu kunionyesha sehemu zake za siri. Niliogopa sana, nilikuwa mdogo, na sikujua la kufanya.”, tukio lililotokea ndani ya treni nyakati za usiku ambapo alinyanyaswa na wasafiri wa kiume.

Akizungumzia mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Dkt. Natalia Kanem amesema, “tunaona uwezekano wa kuwa na dunia ambamo kwayo kila mwanamke na msichana anaweza kuishi bila kukumbana na ukatili wa kingono au ghasia. Tunashirikiana na wadau wetu ili kumaliza adha hii ya ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.”

Kampeni hiyo kupitia simulizi imechapishwa katika watuvi unfpa.org/16days na itaendelea hadi tarehe 10 mwezi ujao wa disemba ambayo ni kilele cha siku ya haki za binadamu duniani.