Maendeleo ya kweli yatapatikana wanawake na wasichana wakiwa huru- Guterres

19 Novemba 2018

Ukatili dhidi  ya wanawake na wasichana ni janga la kimataifa, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wakati akihutubia tukio maalum la siku ya kimataifa ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake lililofanyika kwenye makao makuu ya umoja  huo jijini New York, Marekani hii leo.

Bwana Guterres amewaeleza washiriki kuwa vitendo hivyo vinavyoweka alama ya aibu kwa jamii zote husika, ni kikwazo kikubwa cha kwa maendeleo jumuishi na shirikishi ulimwenguni.

Amesema baya zaidi, vitendo hivyo vinafanyika kila pahali bila kujali kiwango cha maendeleo ya nchi akisema kuwa vimekumba pia taasisi ya Umoja wa Mataifa ambayo anaiongoza, akigusia ukatili wa kingono.

“Na msingi wa ukatili dhidi ya wanawake na wasichana katika aina zote zile, ni mwendelezo wa ukosefu wa heshima- na kushindwa kwa wanaume kutambua usawa na utu wa wanawake. Ukatili ambao mtu amepitia utotoni unahusishwa na yeye kuwepo hatarini zaidi na kukumbwa na ukatili utu uzimani”

Katibu Mkuu amesema hali inakuwa mbaya zaidi pindi taasisi zinaposhindwa kuamini manusura wa ukatili wa wanawake, na kuruhusu watekelezaji wa vitendo hivyo kukwepa mkono wa sheria.

Ametumia jukwaa hilo kupigia chepuo harakati za kijamii za kufichua ukatili dhidi ya wanawake akitolea mfano kampeni ya UNiTE ambayo mwaka huu inaangazia usaidizi kwa manusura na watetezi wa haki za wanawake.

Kampeni imepatiwa jina Pakaza Rangi ya Chungwa, nisikilize nami pia au #OrangeTheWorld:#HearMeToo.

Katibu Mkuu amesema, “tunahitaji usaidizi zaidi kwa manusura na kuwajibisha wahusika. Lakini zaidi ya hapo ni vyema sisi kama jamii tuchukue jukumu la kubadili miundo na tamaduni ambazo zinaruhusu ukatili wa kingono na aina zingine za ukatili wa kijinsia kufanyika.”

Amesema kwa upande wa Umoja wa  Mataifa tayari wanatekeleza usawa wa kijinsia katika  ngazi andamizi za kiongozi na zaidi ya yote kimataifa mfuko wa UN wa kusaidia manusura wa ukatili wa kingono unazidi kuleta nuru.

Mfuko  huo, “unajikita katika kuzuia ukatili, kutekeleza sheria na sera na kuongeza fursa kwa manusura kupata huduma za usaidizi,” amesema Guterres.

Kwa mujibu wa Bwana Guterres, kwa zaidi ya miongo miwili iliyopita, mfuko huo umekuwa na miradi 460 katika nchi 139.

Amegusia pia mpango wa UN na Muungano wa Ulaya, EU wa thamani ya Euro milioni 500 ambao amesema unalenga kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana kwenye nchi 25 za mabara matano.  Mfuko huo “utajengea uwezo manusura na watetezi wa haki za wanawake katika kuelezea simulizi zao na kuwa mawakala wa mabadiliko majumbani mwao, kwenye jamii na hata mataifa yao.”

Bwana Guterres ametamatisha hotuba yake akisema kuwa “dunia katu haitaweza kusema kuwa ina usawa na haki hadi pale nusu ya idadi ya wakazi wake ambao ni wanawake na wasichana, wataishi bila woga na ukatili katika Maisha yao.”

MKURUGENZI MTENDAJI WA UN-WOMEN

Akizungumza katika tukio hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNwomen Phumzile Mlambo-Ngcuka ambaye ndio anaongoza kampeni ya #HearMetoo amesema “sote tunapaswa kuhakikisha kuwa tunaleta utamaduni huu wa mabadiliko na kutokomeza utamaduni ambao unahalalisha manyanyaso dhidi ya wanawake na wasichana.”

Maudhui ya mwaka huu ya siku ya kimataifa ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake tarehe 25 mwezi huu na siku 16 za harakati dhidi ya ukatili wa kijinsia zitakazomalizika tarehe 10 mwezi ujao wa Disemba ni “Pakaza rangi ya chungwa: Nisikilize nami pia au Orange the World: #HearMeToo.

Maudhui haya yanalenga kusaidia manusura wanawake na wasichana kote duniani ambao wamejitokeza na kushikamana dhidi ya ukosefu wa mizania ya kijinsia ambamo kwao ukatili wa kingono umeota mizizi.

Duniani kote, wakati wa siku hizo 16, kutakuwepo na matukio yanayoleta pamoja serikali, jamii, manusura, wanaharakati ili kuhamasisha umma juu ya umuhimu wa dharura wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana kupitia majukwaa ya ngazi ya juu, matukio na kampeni.

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud