Majira ya baridi yakishika kasi, wakazi wa Ukraine mashariki wako hatarini

15 Novemba 2018

Kadri viwango vya nyuzi joto vikizidi kuporomoka huko barani Ulaya, Umoja wa Mataifa umepazia sauti kilio cha wakazi wa maeneo ya mashariki mwa Ukraine ambako mzozo unaoendelea unakwamisha harakati za kuwafikisha misaada ya kibinadamu ikiwemo vifaa vya kujikinga na baridi kali.

Mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine Osnat Lubrani amesema hayo leo huko Geneva, Uswisi wakati akiwapatia muhtasari nchi wanachama wa umoja  huo kuhusu gharama za kibinadamu na madhara ya mzozo wa kibinadamu huko mashariki mwa Ukraine.

“Mzozo huo umeanza mwaka 2014 na hadi sasa raia wanazidi  kupoteza maisha, majeruhi nao wakihitaji misaada huku usaidizi ukipungua kwa kuwa kile kinachoendelea mashariki ya Ukraine kinaonekana kusahauliwa,” amesema Bi, Lubrani akiongeza kuwa ombi la usaidizi kwa mwaka huu pekee huko Ukraine mashariki limefadhiliwa kwa asilimia 36 tu.

                             Amesema ukosefu wa fedha unamaanisha kwamba mamilioni ya wanawake, wanaume na watoto wanaendelea kunyimwa mahitaji yao ya msingi, akiongeza kuwa, “natoa wito kwa nchi wanachama zionyeshe mshikamano na watu wa Ukraine mashariki na kusaidia kuendelea kuwasaidia kipindi chote hiki cha majira ya baridi kali.”

Bi. Lubrani amesema mahitaji ya kipindi hiki yanaenda sambamba na usaidizi wa kisaikolojia, afya ya akili, kiwewe,  ulinzi, makazi, huduma za maji safi na kujisafi kuondoa vilipuzi vilivyotegwa pamoja na mbinu za kujipatia kipato.

Hata hivyo mratibu mkazi huyo wa Umoja wa Mataifa ameshukuru wahisani ambao wameendelea kutoa msaada ambao mwaka huu pekee wameweza kusaidia zaidi ya raia milioni moja kwa kuwapatia huduma za ulinzi, chakula, msaada wa fedha na pia huduma za afya na elimu.

Tangu mzozo wa Ukraine uanze mwaka 2014, zaidi ya watu 3000 wamefariki dunia.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter