Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwazi kwenye sekta ya madini utafanikisha SDGs- Ripoti

Wachimba dhahabu Ghana
Picha: IRIN/John Appiah
Wachimba dhahabu Ghana

Uwazi kwenye sekta ya madini utafanikisha SDGs- Ripoti

Ukuaji wa Kiuchumi

Uwazi katika usimamizi na uendeshaji wa sekta ya madini ni muhimu ili kuhakikisha sekta hiyo siyo tu inakuwa endelevu na kuchangia kwenye maendeleo bali pia haichafui au kuharibu mazingira.

Mkurugenzi wa Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa ya Afrika, UNECA ofisi ya Afrika ya Kati, Antonio Pedro amesema hayo alipohojiwa na shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa akinukuu ripoti ambayo itachapishwa hivi karibuni kuhusu utawala bora katika sekta ya madini.

Bwana Pedro ambaye ni mmoja wa waandishi wa ripoti hiyo ametolea mfano mtazamo tofauti kati ya wachimbaji wadogo, jamii na wasimamizi kuhusu usimamizi wa sekta hiyo na uhifadhi wa mazingira.

Amesema mkinzano huo unakwamisha harakati za uhifadhi wa mazingira akisema, “inahitajika jukwaa halali la wadau wote ili kufanya mashauriano. Katika ripoti yetu tunataka utekelezaji wa kina wa mkataba wa Aahrus kuhusu kupata taarifa kamili, ushiriki wa umma katika kufanya maamuzi na kupata haki juu ya masuala ya mazingira mambo ambayo ni muhimu katika kuhakikisha majadiliano yoyote ni bora na yanafanikisha kuwekwa kwa mipango endelevu ya usimamizi wa mazingira, mipango ambayo kampuni za madini zinapaswa kutekeleza kwa kina na wananchi wasimamie ipasavyo pamoja na serikali.”

Bwana Pedro amesema mikakati ya namna hiyo inaweka pia fursa ya kuhakikisha kampuni husika zinawajibika iwapo kuna ukiukwaji wa kanuni za uendeshaji hata baada ya miradi kukamilika.

Alipoulizwa kuhusu hofu ya ongezeko la athari za uchimbaji madini kwenye mazingira sambamba na mchakato wa kuboresha madini hayo, Bwana Pedro amesema “mara nyingi mbinu za uhifadhi wa mazingira kwenye sekta ya madini zimejikita katika maeneo ya machimbo pekee, na kusahau mnyororo mzima wa kuongeza thamani. Ili kushughulikia jambo hili tunachechemua matumizi ya mfumo mzima wa tathmini ya athari ya mchakato mzima wa madini kuanzia uchimbaji wake hadi kito kinapomfikia mtumiaji.”

Ripoti hiyo imeandaliwa kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili na wataalamu 30 kutoka vyuo vya elimu ya juu, taasisi za utafiti, mashirika ya kimataifa, mashirika ya kikanda, sekta ya viwanda, sekta binafsi na ile ya umma.

Lengo lake ni kuimarisha uelewa wa jinsi ya kusimamia vyema sekta ya madini ili hatimaye iweze kuchangia katika maendeleo endelevu.