Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani wa kwanza kutoka Vietnam watua Sudan Kusini

Wanawake na watoto wa Sudan Kusini wakiwasili katika kambi iliyoko Bentiu humo humo nchini mwao.
UNICEF/Sebastian Rich
Wanawake na watoto wa Sudan Kusini wakiwasili katika kambi iliyoko Bentiu humo humo nchini mwao.

Walinda amani wa kwanza kutoka Vietnam watua Sudan Kusini

Amani na Usalama

Walinda amani kutoka Vietnam wamewasili nchini Sudan Kusini tayari kujiunga na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, UNMISS. Hii ni mara ya kwanza kwa Vietnam kushiriki katika operesheni za ulinzi wa amani.

Wakiwa wamevalia mavazi ya kijeshi, vizibao na kofia zao za buluu zikiwa zimeandikwa herufi mbili, UN, yaani Umoja wa Mataifa, walinda amani 30 ambao ni madaktari na wauguzi kutoka Vietnam wamewasili Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini.

Mara baada ya kutua mjini Juba, ukaguzi wa masuala ya uhamiaji ulifanyika sambamba na kuwapima iwapo wana ugonjwa wa Ebola au la.

Walinda amani  hawa wanatarajiwa kutoa huduma za dharura, uokozi, usaidizi katika upasuaji na huduma ya matibabu ya meno, .

Kamanda mkuu wa kikosi hiki ni Luteni Kanali Bui Duc Thanh

“Vietnam ni  nchi rafiki sana kwa kila mtu duniani kote na Vietnam nayo inataka kuchangia uwezo wake wote katika operesheni za ulinzi wa amani duniani.”

Walinda amani hawa pamoja na wengine wanaotarajiwa kuwasili Sudan  Kusini wiki ijayo wataelekea mji wa Bentiu ulio kaskazini mwa Sudan Kusini. Wataelekea eneo hilo pamoja na vifaa vyao vya matibabu, jenereta, magari ya wagonjwa na yale ya kunyanyua vifaa vizito.

Luteni Samina Ngol ambaye ni mwanajeshi katika kikosi hiki cha walinda amani kutoka Vietnam hakuficha hisia zake.

“Sisi ni wanajeshi. Sasa hivi tunajisikia heshima na tunajivunia kwamba tuko hapa na tunafurahi sana kwa ajili ya jukumu letu la mwaka wetu mmoja ujao kutimiza mpango wa msaada kwa kibinadamu”

Walinda amani hawa kutoka Vietnam watachukua nafasi ya vikosi vya Uingereza ambavyo vilianzisha hospitali iliyokuwa ikihudumia wafanyakazi wa  UNMISS huko Bentiu.