Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola milioni 17 kukwamua vijana Ukanda wa Gaza

Kijana akitazama mandhari ya Jabalia kambi kubwa kabisa kati ya kambi 8 za a wakimbizi Ukanda wa Gaza . Ipo Kaskazini mwa Gaza karibu na kijiji cha Jabalia.
Picha na Suhair Karam/IRIN
Kijana akitazama mandhari ya Jabalia kambi kubwa kabisa kati ya kambi 8 za a wakimbizi Ukanda wa Gaza . Ipo Kaskazini mwa Gaza karibu na kijiji cha Jabalia.

Dola milioni 17 kukwamua vijana Ukanda wa Gaza

Ukuaji wa Kiuchumi

Benki ya Dunia imetangaza mkopo nafuu wa dola milioni 17 kwa ajili ya mradi wa kusaidia vijana wasio na ajira huko ukanda wa Gaza Mashariki ya kati kujipatia kipato na kuweza kuajirika.

Taarifa iliyotolewa na benki hiyo hii leo huko Washington, DC nchini Marekani inasema mradi huo unalenga vijana 4,400 nusu yao wasichana ambapo wataajiriwa na mashirika yasiyo ya kiserikali ili kutoa huduma muhimu kwa ujira kwenye maeneo ya afya, elimu na kusaidia wazee.

Halikadhalika mradi huo utatumika kupatia mafunzo ya stadi pamoja na ajira kupitia mtandaoni kwa vijana wengine 750 ambao wote wana umri wa kati ya miaka 18 hadi 34.

Mkurugenzi wa Benki ya Dunia katika ukingo wa magharibi wa mto Jordan pamoja na ukanda wa Gaza Marina Wes amesema kupitia mradi huo vijana watalipwa ujira kwa kazi wanazofanya na hivyo kuweza kukimu familia zao.

Amesema kwa wale watakaopata mafunzo ya biashara mtandao, wanaweza kuanzisha biashara na hata wengine kuwa waandishi wa kujitegemea wa mtandaoni huku wengine wakifanya kazi za kukusanya takwimu zinazohitajika.

Watu 900,000 ukanda wa Gaza ambao ni nusu ya idadi ya wakazi aw eneo hilo ni maskini ambapo 300,000 kati yao ni hohehahe wasio na  uwezo wa kukimu mahitaji ya malazi, chakula na mavazi.