Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde lindeni wahudumu wa kibinadamu Syria- Moumtzis

Vituo vya kujihifadhi huko jimbo la Dara'a nchini SYria.
UNHCR/Bassam Diab
Vituo vya kujihifadhi huko jimbo la Dara'a nchini SYria.

Chonde chonde lindeni wahudumu wa kibinadamu Syria- Moumtzis

Msaada wa Kibinadamu

Umoja wa Mataifa umerejea wito wake wa kutaka ulinzi na usalama kwa watoa huduma za misaada nchini Syria, ambao bado wamesalia mstari wa mbele wa mapambano wakitoa misaada adhimu kwa mamilioni ya wanawake, watoto na wanaume waliosalia nchini humo.

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa kwa janga la Syria Panos Moumtzis amesema hayo leo huko Amman nchini Jordan wakati huu ambapo licha  ya mapigano kushika kasi, wahudumu hao wamejitolea kutwa kucha kuokoa maisha ya binadamu.

Nchini Syria watu wapatao milioni 13 wanahitaji misaada ya kibinadamu wakiwemo milioni 6.5 ambao ni wakimbizi wa ndani kwenye maeneo yanayoshikiliwa na serikali na vikundi vya upinzani.

“Watoa misaada ya kibinadamu wanahatarisha maisha yao kila siku na wanafanya kazi bila kuchoka kusambaza misaada ya kibinadamu kwa wasyria wenzao kwa mujibu wa misingi ya kibinadamu,” amesema Bwana Moumtzis huku akisema pande zote kinzani nchini Syria zina wajibu wa kulinda wafanyakazi hao na raia kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu pamoja na haki za binadamu.

Mratibu huyo amesema licha ya pande hizo kupaswa kuwajibika, bado wahudumu hao wako katika hatari kubwa ya kukamatwa na kuswekwa rumande wakati wakiwa kazini wakati huu ambapo udhibiti wa maeneo unabadilika mara kwa mara.

Ametolea mfano eneo la kusini-magharibi mwa Syria ambako wahudumu wengi wa misaada wameacha kufanya kazi zao na hivyo kuacha ombwe kubwa la usaidizi kwa raia.

Amesema ni muhimu hatua zote zikachukuliwa ili kuongeza ulinzi kwa wahudumu hao wa kibinadamu na kuhakikisha kuwa  huduma wanazotoa zinaendelea.

Umoja wa Mataifa unasema Syria ni eneo hatari zaidi kwa watoa huduma za kibinadamu kufanya kazi zao ambapo tangu vita ianze mwaka 2011 mwezi machi, mamia ya wafanyakazi hao na watoa huduma za afya wameuawa wakiwa kazini.