Guterres aunda jopo kuhakikisha maendeleo ya kidijitali yana manufaa kwa wote

12 Julai 2018

Jopo la ngazi ya juu lenye jukumu la  kuhakikisha kuwa maendeleo ya teknolojia ya kidijitali  yananufaisha wakazi wote wa dunia, limetangazwa hii leo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres.

Jopo hilo la ngazi ya juu kuhusu ushirikiano wa kidijitali litakuwa na wenyeviti wenza wawili ambao ni Melinda Gates kutoka taasisi ya Bill na Melinda Gates, na mwanzilishi wa kampuni ya Alibaba Jack Ma huku wajumbe wakiwa ni 18 wakitoka nyanja za viwanda, mashirika ya kiraia na elimu.

Balozi Amandeep Gill ambaye yuko kwenye sekretarieti ya jopo hilo amesema kuwa Katibu Mkuu Guterres anataka kuepusha mwelekeo wa ushindani katika masuala ya kidijitali ambayo kwa sasa yanaathiri mashauriano ya biashara, data na usalama.

“Dhana hiyo ya ushindani inaweza kuzuia sekta hii kuchangia vyema kwenye kufanikisha ajenda 2030 ya maendeleo endelevu,” amesema Balozi Gill akizungumza huko Geneva, Uswisi.

Amesema ni kwa mantiki hiyo ni muhimu kuwepo kwa jopo la pamoja ambalo litaweza kubonga bongo kuhusu manufaa na madhara ya maendeleo ya kidijitali kiuchumi, kijamii na kwenye haki za binadamu.

Jopo hilo litafanya kazi kwa miezi 9 ambapo wajumbe wake watakutana kwa mara ya kwanza jijini New York, Marekani wakati wa mjadala wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba mwaka huu na baadaye huko Geneva, Uswisi mwezi Januari mwakani.

Wajumbe wa jopo hilo kutoka Afrika ni watatu ambao ni Bogolo Kenewendo, Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda wa Botswana,  Akaliza Keza Ntwari, mchechemuzi wa TEHAMA na mjasiriamali kutoka Rwanda na Nanjira Sambuli kutoka taasisi ya World Wide Web ya nchini Kenya.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter