Usawa wa kijinsia ni muhimu ili teknolojia ya kidijtali iwe na manufaa zaidi

10 Juni 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres leo amepokea ripoti ya jopo la ngazi ya juu alilounda kuhusu masuala ya ushirikiano wa kidijitali, ripoti ambayo amekabidhiwa na wenyeviti wenza wa jopo hilo Melinda Gates wa taasisi ya Bill and Melinda Gates na Jack Ma ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa kundi la Alibaba.

Punde tu baada ya kupokea ripoti hiyo Katibu Mkuu pamoja na Jack Ma na Melinda Gates walishiriki mjadala wa mtandaoni wakijadili ripoti hiyo ambapo Guterres amesisitiza umuhimu wa ujumuishi katika maendeleo ya kidijitali akisema kuwa utandawazi bado haujawa na manufaa kwa kila mtu na zaidi ya yote maendeleo ya kidijitali yameongeza pengo la ukosefu wa usawa.

Katibu mkuu amesema “pindi ninapoangalia ajenda 2030, lengo letu ni kutomwacha nyuma mtu yeyote, kuwa na utandawazi sawia na kuna njia moja tu ya kufanikisha, ambayo ni kutumia kadri tunavyoweza teknolojia ili kuweka mizania ya uhusiano kati ya maendeleo duniani na maendeleo sawia. Lakini hilo lifanyike, kuna tishio kubwa ambalo tunapaswa kukabili; nusu ya wakazi wa dunia hawako kwenye mtandao.”

Kwa upande wake, Melinda amezungumzia nafasi ya jinsia katika mjadala wa mfumo wa dijitali akiasema, “wanawake wanapaswa siyo tu kuwa na ufahamu wa masuala ya kidijitali ili waweze kunufaika na mifumo ya utumaji fedha kwa njia ya mtandao au waweze kuweka akiba ya fedha yao wanapokuwa maeneo ya mbali bali pia ili waweze kushiriki kwenye mazungumzo na kutoa uamuzi.”

Ametoa mfano wa Malawi akisema, ukiweza kuweka akiba ya dola moja kwa siku. Inaleta tofauti kubwa sana tunafahamu kwenye afya na ustawi na elimu ya familia iwapo mwanamke anaweza kunufaika na huduma hizo.

Melinda amesema huduma hizo ziko maeneo mengi hivi sasa duniani kwa hiyo pamoja na uwepo wa huduma, wanawake wapate fursa ya kushiriki maamuzi kuhusu huduma hizo.

Halikadhalika amesema ingawa teknolojia ya kidijitali ipo na inabadilika mara kwa mara kiasi kwamba huwezi kujua kitakachofanyika kesho , bado hakuna miundombinu ya kutosha hususan kwenye usimamizi ili teknolojia hiyo iweze kutumika ipasavyo.

Bwana Ma yeye akasema kuwa, “miaka 30 au 40 ijayo, tutatengeneza mashine kama binadamu. Sasa tunaweza vipi kubadili mfumo wetu wa elimu ili tuhakikishe kuwa watoto wetu wanaweza kushindana na roboti, kompyuta, akili bandia, yaani si tu kutumia ubongo bali pia kutumia moyo ili wawe wabunifu na wagunduzi zaidi.”

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud

Fuatilia Habari: Habari zilizopita za Mada Hii

Ushirikiano na haki za binadamu ni nguzo katika ulimwengu wa kidijitali:UN

Jopo la ngazi ya juu la Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya ushirikiano wa kidijitali leo limewasilisha ripoti yake kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu “Mustakabali salama na jumuishi” katika zama hizo za kidijitali.