Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushirikiano na haki za binadamu ni nguzo katika ulimwengu wa kidijitali:UN

Pengo la teknolojia ya dijitali bado ni kikwazo duniani.
ITU
Pengo la teknolojia ya dijitali bado ni kikwazo duniani.

Ushirikiano na haki za binadamu ni nguzo katika ulimwengu wa kidijitali:UN

Masuala ya UM

Jopo la ngazi ya juu la Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya ushirikiano wa kidijitali leo limewasilisha ripoti yake kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu “Mustakabali salama na jumuishi” katika zama hizo za kidijitali.

Ripoti ya jopo hilo linaloongozwa na Melinda Gates mwenyekiti mwenza wa wakfu wa Bill na Melinda Gates na Jack Ma, mwenyekiti mtendaji wa kampuni ya Alibaba inasisitiza umuhimu wa kutomwacha yeyote nyuma katika zama hizo za kidijitali na jinsi gani ushirikiano na teknolojia vinaweza kuchangia katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu ,SDGs.

Ripoti hiyo inataka kuwe na ushirikiano wa kimataifa katika matumizi ya takwimu na maendeleo ya kidijitali kwa umma ili kusaidia kusongesha juhudi za kufikia SDGs kwa kuwezesha teknolojia za kidijitali kutumika kama kipimo.

Miongoni mwa masuala hayo ya kidijitali na teknolojia yaliyoainishwa na ripoti hiyo ni “huduma ya fecha kwa njia ya mtandao wa simu, utambuzi wa kidijitali na huduma za serikali, biashara mtandaoni na kurahisisha upatikanaji wa huduma ya intaneti”.

Fursa za huduma na teknolojia

Pia ripoti imesisitiza ukweli kwamba takribani nusu ya watu wote duniani bado hawana fursa ya huduma za intaneti au inatumia sehemu ndogo tu ya huduma hiyo japo imeunganishwa na mtandao.

Mbali ya fursa changamoto zingine zinazojitokeza katika zama hizo za kidijitali jopo hilo linasema ni masuala ya haki za binadamu , uharaka wa kibinadamu, imani na usalama. Pia imesisitiza tatizo kubwa la tarifa na mambo yenye athari katika mitandao ya kijamii, changamoto za uhuru wa faragha na umuhimu wa uaminifu na utulivu katika mazingira ya kidijitali.

Nini kifanyike

Ripoti ya jopo hilo imetoa wito wa kuchukua hatua madhubuti kuzuia kumomonyoka kwa imani na utulivu kunakotokana na matumizi mabaya ya uweze wa teknolojia na masuala ya kidijitali.

Na kuhusu suala nyeti la akili bandia au AI, jopo hilo limependekeza kwamba mifumo ya akili bandia itengenezwe katika mfumo ambao maamuzi yake yanaweza kuelezewa na binadamu kuwajibika na matumizi yake. Pili limetoa wito wa kuimarishwa kwa mfumo wa kimataifa wa ushirikiano katika masuala ya kidijitali , tatu ripoti imebainisha mapengo na changamoto katika mwenendo wa sasa na kupendekeza mambo ambayo yanaweza kusimamia na kudhibiti mfumo huo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo jumuiya ya kimataifa haihitaji kuanza mwanzo kabisa inaweza kuendeleza mifumo ambayo tayari ipo kwa ajili ya ushirikiano wa kidijitali ikiwemo majukwaa na mitandao ya serikali, sekta, mashirika ya teknolojia, asasi za kiraia pamoja na taratibu na kanuni zilizopo, kama vile sheria, utamaduni, mwongozo na taratibu za kiutendaji.

Mapendekezo

Jopo hilo la kimataifa limependekeza masuala muhimu matano katika kufanikisha dhamira ya teknolojia na zama za kidijitali kwa wote.

Mosi: kujenga uchumi na jamii jumuishi za kidijitali

Pili: Kuwajengea uwezo binadamu na taasisi husika

Tatu: Kulinda haki za binadamu na uharaka wa kibinadamu

Nne: Kuchagiza Imani, usalama na utulivu wa kidijitali

Tano: Kukumbatia na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa wa kidijitali.