Uagizaji chakula nje ya nchi bado ni mzigo kwa mataifa masikini -FAO

11 Julai 2018

Kuagiza chakula kutoka nje kunaongeza  mzigo mkubwa kwa mataifa maskini duniani, imesema ripoti mpya kuhusu hali ya chakula iliyotolewa na  shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa la FAO

Mathalani kwa ujumla tangu mwaka 2000 hadi mwaka jana, mataifa duniani yalitumia dola trilioni 1.43 kuagiza chakula nje ya nchi, kiwango ambacho ni ongezeko mara tatu huku gharama ikiwa imepanda mara tano zaidi kwa mataifa ambayo  yanakabiliwa na zaidi na uhaba wa chakula.

Adam Prakash, mchumi wa FAO na mwandishi wa ripoti hiyo amesema kuwa hali hii inaonyeshamwenendo ambao umekuwa ukipungua kwa muda na kuongeza changamoto hususan kwa mataifa maskini katika kuweza kukidhi mahitaji yao ya chakula kutoka masoko ya kimataifa.

Ripoti inaonya kuwa gharama zinaweza kupanda zaidi mwaka huu kwa kiwango cha  asilimia  3 na kufika  dola trilioni 1.47.

 

Mkulima wa baada ya mavuno Bangladesh. FAO yamsema mataifa maskini yatumia pesa nyingi kuagizia chakula kama mchele.
Picha: IFAD/GMB Akash
Mkulima wa baada ya mavuno Bangladesh. FAO yamsema mataifa maskini yatumia pesa nyingi kuagizia chakula kama mchele.

Kwa nchi zinazoinukia kiuchumi, LDCs, ripoti inasema kuwa hutumia asilimia 28 ya pato la mauzo ya nje kuagiza chakula kutoka nje ya nchi.

Ongezeko hilo la mwaka linaakisi biashara kubwa ya kimataifa ya samaki, chakula ambacho kinaagizwa zaidi na nchi tajiri pamoja na nafaka ambazo ni mlo tegemezi kwa nchi za kipato cha chini zinazokabiliwa na uhaba wa chakula.

Ripoti inasema kuwa mwaka huu FAO ilichunguza muda mrefu wa mwenendo huo na kugundua kwamba  mataifa huenda yanalipa pesa nyingi kununua chakula kidogo, ijapokuwa uzalishaji duniani pamoja na mazingira ya mauzo hayakuwa mabaya sana  katika kipindi cha miaka hii michache.

Halikadhalika ripoti hii inayochapishwa mara mbili kwa mwaka imetenga sura maalum kuhusu ongezeko la biashara ya matunda ya maeneo ya tropiki ambayo awali hayakupatiwa kipaumbele.

Matunda hayo ni pamoja na mapera ilhali awali matunda  yaliyopatiwa kipaumbele yalikuwa maembe na mapapai.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter