Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sitisheni mapigano Syria –Guterres

Uharibifu katika mji wa Homs, Mashariki mwa Syria. Syria ni nchi isiyo na amani zaidi duniani
UNICEF/Penttila
Uharibifu katika mji wa Homs, Mashariki mwa Syria. Syria ni nchi isiyo na amani zaidi duniani

Sitisheni mapigano Syria –Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, amesikitishwa na  muendelelezo wa mashambulizi ya kijeshi  unaoendelea nchini Syria, ukiambatana na mashambulizi kutoka angani na makombora mazito kusini-magharibi mwa nchi hiyo.

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake hii leo jijini New York, Marekani,

Bwana Guterres amesema kuwa mashambulio hayo yamesababisha maelfu ya raia kukimbia makazi  yao, huku wengi wao wakielekea mpakani mwa Syria na Jordan.

Amesema pamoja na hayo, ana hofu juu ya madhara ya muendeleo wa  mashambulizi hayo kwa usalama wa kikanda.

Ametilia mkazo hali ngumu inayokabili raia  huko kusini mwa Syria na  amesihi kukomeshwa haraka kwa muendelezo wa mashambulizi hayo huku akiwahimiza wadau kuheshimu majukumu yao chini ya sheria za kimataifa na pia sheria za kimataifa za kibinadamu ikiwemo kulinda raia wa kawaida pamoja na miundombinu ya kiraia.

Akirejelea makubaliano ya kuacha muendelezo wa mapigano na sitisho la mapigano ambayo yalileta utulivu kusini-magharibi mwa Syria katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja uliopita, Katibu Mkuu amesihi pande zote kujizuia na pia kupatia kipaumbele suala la kuheshimu ahadi zao.