Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua mpya zahitajika kudhibiti jangwa na ukame- FAO

Ukame  unazidi kuathiri ardhi ya sehemu kubwa katika  bara la Afrika.
UNICEF/Mukwazhi
Ukame unazidi kuathiri ardhi ya sehemu kubwa katika bara la Afrika.

Hatua mpya zahitajika kudhibiti jangwa na ukame- FAO

Tabianchi na mazingira

Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limetoa wito katika ripoti mpya iliyotolewa hii leo wa mabadiliko ya kimsingi wa mwelekeo wa jinsi nchi zinavyochukulia na kushughulikia ukame katika ukanda wa mashariki na kaskazini mwa bara la Afrika.

FAO imesema mwelekeo wa kuchukua hatua mapema kwa kuzingatia misingi ya kupunguza madhara unahitajika ili kujenga mnepo zaidi wa jamii wakati wa ukame.
“Ijapokuwa ukame ni jambo lilizoeleka kwenye ukanda huo, katika miongo minne iliyopita, ukame umeenea zaidi, umedumu kwa muda mrefu na kutokea mara kwa mara, penginepo kutokana na mabadiliko ya tabianchi,” imesema ripoti hiyo.
Ripoti inasema licha ya ukame kuwa jambo la kawaida, bado hakuna msisitizo wa kutosha ya jinsi ya kujikwamua baada ya ukame, “tumesalia kuwa waathirika wa ukame, fedha si za ku tosha, kujiandaa kusikotosheleza na uratibu unabakia kuwa kikwazo,” imeonya ripoti hiyo.
Mathalani katika eneo hilo la mashariki na kaskazini mwa Afrika, wakulima na wachungaji wanakabiliwa na changamoto kubwa kadri maji yanavyozidi kutoweka, ongezeko la mmomonyoko wa udongo na udongo usyo na rutuba.
Ripoti inapendekeza hatua kadhaa ikiwemo kueneza teknolojia za kukabiliana na ukame na kuunga mkono sera na hatua ambazo zitashawishi matumizi bora ya ardhi na maji.
Akizungumzia ripoti hiyo, Bwana Reno Gastro ambaye ni Mkurugenzi Mkuu msaidizi, akihusika na idara ya ardhi ,maji na  hali ya hewa ya FAO amesema kuna umuhimu wa kubadili mwelekeo wa jinsi ya kutambua na  kusimamia tatizo la ukame kwa kuondokana na mfumo kwa dharura pekee uliozoeleka na kuweka sera za kuchukua hatua mapema na kupanga  mipango ya muda mrefu ili kupunguza athari na kujenga mnepo zaidi katika siku za usoni.
Aidha Bw. Garstro amesema kwamba kuendeleza na kutekeleza sera za usimamizi wa ukame wa kitaifa kulingana na malengo ya maendeleo ya nchi pamoja na kuanzisha mifumo ya onyo la mapema ni muhimu.
Mkurugenzi Mkuu huyo msaidizi amesema ripoti hiyo mpya ya iliyozinduliwa kabla ya siku ya kupambana na kuenea kwa jangwa na ukame duniani tarehe 17 mwezi huu,  inatathmini upungufu katika usimamizi wa tatizo la ukame wa sasa , na pia kutoa mapendekezo ya kusaidia serikali katika  kurekebisha sera na mipangilio ya kujiandaa kwa kutoa suluhisho zinazozingatia mazingira ya kila nchi.
FAO na pamoja na taasisi ya chakula na maji ya Daugherty ya Chuo Kikuu cha Nebraska ndio waasisi wa ripoti hiyo inayozihusisha   nchi 20 na maeneo ikiwemo Algeria, Bahrain, Misri, Iraq, Iran, Jordan, Kuwait, Lebanon, Libya, Mauritania, Morocco, Oman, Palestina, Qatar, Saudi Arabia, Sudan, Syria, Tunisia, Falme za kiarabu-UAE, na Yemen.